
Na Lucy Ngowi
BODI ya Bima ya Amana (DIB) imesema wananchi waliokuwa na amana katika benki zitakazofungwa au kufutiwa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hulipwa fidia ya amana zao zilizo katika kiwango cha kinga ndani ya mwezi mmoja baada ya kutangazwa rasmi kufutwa kwa leseni ya benki husika.
Akizungumza kuhusu hilo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa DIB, Lwaga Mwambande, alisema kiwango cha juu cha amana kinachokingwa na bodi hiyo ni Sh milioni 7.5 kwa kila mteja.
Alifafanua kuwa mteja yeyote mwenye amana isiyozidi kiwango hicho hulipwa fedha zake zote endapo benki yake itafungwa au kufutiwa leseni.
Hata hivyo, alisema kwa wateja wenye amana zinazozidi Sh milioni 7.5, DIB huendesha zoezi la ufilisi ili kudhibiti na kuuza mali za benki husika kwa lengo la kurejesha sehemu ya amana zao.
Mwambande alitoa mfano wa Benki ya FBME iliyofutiwa leseni mwaka 2017, akisema katika awamu mbili zilizopita walilipwa jumla ya asilimia 55 ya madai yao, na novemba 2025 yametangazwa malipo mengine ya asilimia 30, na hivyo kufanya wawe wamelipwa jumla ya asilimia 85 ya madai yao.
Aliongeza kuwa DIB inaendelea kukusanya na kusimamia mali za benki zilizofungwa ili kuhakikisha wateja wanarejeshewa kiwango kikubwa zaidi cha fedha zao kadri inavyowezekana.
Aidha, alisema kuwa kuanzia mwaka jana, bodi hiyo imeanza kutekeleza jukumu la kupunguza hasara mapema kwa kuingilia kati kabla benki haijafikia hatua ya kufilisika au kufutiwa leseni.
Kupitia ushirikiano na Benki Kuu ya Tanzania, DIB inaweza kuidhinisha mikopo au kusaidia kuikopesha benki yenye changamoto ili kurejesha uimara wake wa kifedha na kuiwezesha kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.


