Na Geofrey Stephen Arusha .
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Amos Makala, ameongoza hafla fupi ya kukabidhi hundi yenye thamani ya shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi waliopisha ardhi yao kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu utakaotumika katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Hafla hiyo imefanyika mkoani Arusha na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Joseph Mkude, wataalamu kutoka sekta ya ardhi, pamoja na wananchi wanufaika wa fidia hiyo. Tukio hilo ni ishara ya dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha haki za wananchi zinalindwa wakati wa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ya taifa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Amos Makala alisema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha miradi ya kimkakati inatekelezwa sambamba na kulinda maslahi ya wananchi. Alisisitiza kuwa malipo ya fidia ni haki ya msingi na yanapaswa kulipwa kwa wakati, kwa uwazi na kwa mujibu wa sheria.
“Maendeleo hayawezi kusimama, lakini hayawezi pia kuwanyanyasa wananchi. Ndiyo maana leo tunakabidhi fidia hii kwa wananchi waliopisha ujenzi wa uwanja wa AFCON 2027,” alisema Mhe. Makala.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Joseph Mkude, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais kwa kuleta mradi mkubwa wa ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu mkoani Arusha.
Alisema mradi huo ni wa kihistoria na utaleta manufaa makubwa kwa wakazi wa Arusha na taifa kwa ujumla.
Mhe. Mkude alibainisha kuwa ujenzi wa uwanja huo utafungua fursa za ajira kwa vijana, kukuza sekta ya michezo, kuimarisha utalii na kuongeza mzunguko wa uchumi katika Mkoa na Wilaya ya Arusha. Aidha,
aliwashukuru wananchi waliopisha ardhi kwa moyo wao wa uzalendo na ushirikiano waliouonesha kwa serikali.
Mwisho .



