Siha, Kilimanjaro –
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imemtangaza mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Godwin Mollel, kuwa Mbunge wa Jimbo la Siha baada ya kushinda uchaguzi uliofanyika Desemba 30, 2025.
Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo usiku huo, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Siha, Marko Masue, alisema Dk Mollel amepata kura 51,769, sawa na asilimia 78.4 ya kura zote zilizopigwa.

Mpinzani wake wa karibu, Ntaana Thobias wa chama cha NRA, alipata kura 4,992 sawa na asilimia 7.56. Mgombea wa ACT Wazalendo, Ashukuriwe Matemu, alipata kura 3,678 (asilimia 5.57), huku Mdoe Yambazi wa chama cha Sauti ya Umma (SAU) akipata kura 3,128 (asilimia 4.74). Mgombea wa chama cha Makini, Daniela Msila, alipata kura 2,007, sawa na asilimia 3.04.
“Kwa mujibu wa matokeo haya, namtangaza rasmi Dk Godwin Mollel wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa ndiye mshindi wa kiti cha ubunge wa Jimbo la Siha,” alisema Msimamizi wa Uchaguzi.

Uchaguzi huo uliahirishwa awali baada ya kifo cha aliyekuwa mgombea wa CUF, Daudi Ntuyehabi, aliyefariki dunia Oktoba 7, 2025, katika tukio lililoripotiwa kuhusisha shambulio dhidi yake.
Kwa upande wake, Joseph Mbena, Mwenyekiti wa chama cha NRA Mkoa wa Kilimanjaro, alimpongeza Dk Mollel kwa ushindi huo, akisisitiza kuwa ushindi huo ni wa wananchi wa Siha.

“Tunampongeza kwa ushindi alioupata, lakini huu ni ushindi wa wananchi wa Siha, si wake binafsi,” alisema Mbena.
Aliongeza kuwa jambo la msingi kwa mbunge mpya ni kuhakikisha anatimiza ahadi alizotoa wakati wa kampeni na kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia mahitaji yao.
Mwisho .



