Hai, Kilimanjaro –
Maadhimisho ya Maulidi ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SWA) yanatarajiwa kufanyika kimkoa kwa siku tatu Wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, kuanzia Januari 1 hadi Januari 3, 2026. Maadhimisho hayo yataenda sambamba na kumbukizi ya miaka 57 ya kuanzishwa kwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
Akizungumza na vyombo vya habari tarehe 28 Desemba 2025 huko Bomang’ombe, Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaabani Mlewa, amesema kuwa hafla hiyo itahusisha wahadhiri mbalimbali, masheikh kutoka mikoa tofauti pamoja na viongozi wa Serikali.

Sheikh Mlewa amewaomba Waislamu kujitokeza kwa wingi kushiriki hadhara hiyo itakayofanyika katika Msikiti Mdogo Uzunguni, Bomang’ombe. Amefafanua kuwa masheikh kutoka mikoa ya Arusha, Tanga, Manyara, Singida na Mwanza wanatarajiwa kushiriki na kutoa muhadhara katika siku zote za maadhimisho.
Ratiba ya Maadhimisho
Alhamisi, Januari 1, 2026
Siku ya uzinduzi rasmi wa hadhara hiyo itatanguliwa na Itikafu kubwa itakayofanyika katika Msikiti Mkubwa wa Shafii, Bomang’ombe. Katika Itikafu hiyo kutafanyika dua maalum ya kuliombea Taifa, kuombea amani ya nchi, na kumuomba Mwenyezi Mungu alinde na kuijalia salama Tanzania.
Ijumaa, Januari 2, 2026
Maadhimisho yataendelea kwa shughuli mbalimbali ikiwemo utoaji wa chakula cha mchana kwa makundi mbalimbali kama vile masikini, bodaboda, wapiga debe wa stendi, vijana wa misikiti na wananchi wengine. Pia kutakuwa na hotuba, mashindano ya kusoma Qur’an, kaswida pamoja na michezo mbalimbali.
Jumamosi, Januari 3, 2026.

Siku ya mwisho itahusisha maandamano makubwa ya jioni yanayoambatana na Maulidi. Sheikh Mlewa amesema tukio hilo litakuwa sehemu ya kuadhimisha miaka 57 ya BAKWATA na kuonyesha kazi, mafanikio na maendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wa Mufti Abubakar Zubeir.
Ameeleza kuwa ni fursa muhimu kwa Waislamu kujifunza na kufahamu mambo mengi mazuri ambayo BAKWATA imeyafanya kwa muda mrefu, pamoja na kuelewa majukumu yake katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Maoni ya Waumini.
Mmoja wa waumini wa Kiislamu mkazi wa Bomang’ombe, Bakari Hamisi, ameishukuru BAKWATA Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuleta maadhimisho ya Maulidi Wilayani Hai. Amesema tukio hilo litawawezesha waumini kujifunza mambo mengi kupitia wahadhiri, masheikh na viongozi watakaotoa nasaha, hususan kuhusu kulinda amani na mshikamano wa Taifa.
Mwisho.



