Na Bahati Hai .
Wananchi wa kijiji cha Mkombozi, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, wamemwomba Mkuu wa Wilaya hiyo, Hassan Bomboko, kufanya ziara katika kijiji chao ili kujionea uharibifu wa vyanzo vya maji unaodaiwa kufanywa na wafugaji wanaoingiza mifugo katika maeneo hayo.
Ombi hilo limetolewa katika mkutano wa kufunga mwaka uliofanyika kijijini hapo, ambapo wananchi walisomewa taarifa mbalimbali za maendeleo pamoja na taarifa ya mapato na matumizi.


Wakizungumza Desemba 24, 2025, wananchi wamesema kuwa mifugo imekuwa ikiingizwa katika vyanzo vya maji vinavyotumika kwa matumizi ya nyumbani na kilimo cha umwagiliaji, hali inayosababisha uharibifu wa mazingira, kukauka kwa maji na kuharibika kwa mifereji ya umwagiliaji.
“Katika kijiji hiki, asilimia kubwa ya wananchi tunategemea kilimo cha umwagiliaji. Kuletwa kwa mifugo kwenye vyanzo vya maji kumesababisha mazao kukauka na kuharibu mazingira,” wamesema wananchi hao.
Wananchi hao wamesisitiza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akihimiza uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji, hivyo vitendo vya wafugaji hao vinakwenda kinyume na juhudi za Serikali.
Mwananchi mmoja, Braison Ulotu, amesema kuwa maeneo yaliyoathirika ni pamoja na Zarahu, Kambi ya Chura na Tindigani, huku akidai mifugo hiyo hupitia kijiji cha Sadala kabla ya kuingia Mkombozi.
Kwa upande wake, Fadhila Munisi amesema wananchi wameamua kutumia busara kwa kuiomba Serikali iingilie kati, kwani baadhi ya wafugaji wamekuwa wakitishia kuwachapa bakora wanaojaribu kuwazuia, hali inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Julius Mallya, amesema changamoto zote zilizotajwa zitafanyiwa kazi, ikiwemo suala la mifugo kuingia katika vyanzo vya maji. Pia ametaja hatua zilizochukuliwa kudhibiti unywaji wa pombe nyakati za kazi, wizi wa majumbani, matumizi ya dawa za kulevya, pamoja na kufuatilia kesi ya fedha za SACCOS iliyopo mahakamani.
Kwa ujumla, uongozi wa kijiji umeahidi kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha changamoto zote zinafanyiwa kazi ili wananchi waendelee kuishi kwa amani na kuendelea na shughuli zao za maendeleo.
Mwisho .



