Watanzania Wametakiwa Kuwajenga Watoto katika Maadili Mema kama Kinga ya Maovu.

Geofrey Stephen
3 Min Read

Na Bahati Hai .

Jamii imetakiwa kuwekeza katika malezi yenye maadili mema na tabia njema kwa watoto, kwani maadili hayo ni msingi muhimu wa kujenga jamii yenye amani, umoja na usalama.

Wito huo umetolewa na Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaabani Mlewa, wakati wa mahafali ya wahitimu wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Kibohehe, iliyopo Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza leo Desemba 13, 2025, katika mahafali hayo yaliyohudhuriwa na viongozi wa dini, Serikali, wadau wa maendeleo pamoja na wazazi na walezi, Sheikh Mlewa alisisitiza umuhimu wa jamii kuanza kuwalea watoto katika misingi ya maadili mema tangu wakiwa wadogo.

Habari Picha 4729
Habari Picha 4728

Amesema kuwa mtoto anayejengewa maadili mema na tabia njema huimarishiwa uwezo wa kutambua mema na mabaya, hali inayomsaidia kuepuka kujihusisha na vitendo viovu.

“Wazazi wanapaswa kujenga msingi imara wa maadili tangu watoto wakiwa wadogo, kwani kama walivyosema wahenga, samaki mkunje angali mbichi,” amesema Sheikh Mlewa.

Aidha, ameeleza kuwa marafiki pamoja na matumizi ya mitandao ya kijamii kama WhatsApp na Instagram ni miongoni mwa sababu kubwa zinazoweza kubadilisha tabia na maadili ya mtoto, kwani mara nyingi watoto hubadilika ili wakubalike kwenye makundi yao ya kijamii.

Kutokana na hilo, amewataka wazazi kuwaandaa watoto wao kimaadili ili wawe na uwezo wa kusimamia misimamo yao hata pale inapokwenda kinyume na ushawishi wa marafiki.

 

Habari Picha 4730
Habari Picha 4731

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa BAKWATA Wilaya ya Hai, Omar Maamudu, amewakumbusha wananchi umuhimu wa kulinda amani ya nchi, akitolea mfano machafuko yanayoendelea katika baadhi ya nchi jirani ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan.

“Tunashuhudia mateso wanayopitia watoto, wanawake na wazee wanaokimbia vita wakiwa wamebeba mizigo vichwani. Hali hii inasikitisha sana. Naomba tutunze amani ya nchi yetu, tusishawishiwe na watu kutoka nje. Amani ikivurugika ni vigumu kuirudisha,” amesema Omar.

Naye Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari Kibohehe, Abdulkaffar Mfinanga, amewataka wazazi kuendelea kusimamia maadili na nidhamu ya watoto wao hata baada ya kuhitimu masomo ya sekondari.

“Watoto hawa wanaporejea nyumbani, wanakuwa chini ya uangalizi wa wazazi wao. Endapo uhalifu wowote utatokea, mzazi ataulizwa. Hivyo mzazi ana wajibu wa kusimamia mwenendo wa mtoto wake,” amesisitiza Mfinanga.

Habari Picha 4732

Ameongeza kuwa mtoto anapokuwa nyumbani bado yupo chini ya uongozi wa mzazi, tofauti na pale anapokuwa amejitegemea, ambapo hupata uhuru mkubwa wa kufanya maamuzi yake binafsi.

Aidha, amewashauri wazazi kutumia kipindi cha kusubiri matokeo kwa kuwapeleka watoto wao kwenye maeneo salama ya kujifunza maadili, stadi za maisha na ujasiriamali, badala ya kuwaacha nyumbani kwa muda mrefu bila shughuli, hali inayoweza kuwafanya kujiingiza katika makundi yasiyofaa.

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment