MAENDELEO MAPYA ARUSHA: BARAZA JIPYA LA MADIWANI LAZINDULIWA KWA HAMASA NA MATUMAINI MAKUBWA YA MABADILIKO KWA WANACHI .

Geofrey Stephen
4 Min Read

Zinduko la Baraza Jipya la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Arusha: Madiwani 34 Waanza Safari ya Kuleta Maendeleo kwa Uwajibikaji na Uadilifu

Baraza Jipya la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha limezinduliwa rasmi mbele ya mamia ya wananchi, likishuhudia kiapo cha utii, uadilifu na uwajibikaji kilicholiwa na madiwani 34—wakiwemo 25 wa kuchaguliwa na 9 wa viti maalum. Hafla hii, iliyoongozwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Boniface Semroki, ilijawa na shangwe na matumaini mapya kutoka kwa wananchi waliokusanyika kushuhudia viongozi wao wakiwa tayari kuanza rasmi majukumu ya utumishi wa umma.

Habari Picha 4636

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude: “Heshimuni Kiapo Chenu, Mtekelezeni kwa Vitendo”

Mara baada ya madiwani kuapishwa, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, alizungumza na kuwataka viongozi wapya kuheshimu kiapo walichokula na kutekeleza kwa vitendo ahadi walizotoa kwa wananchi. Mkude alisisitiza kuwa maendeleo ya kweli yanapatikana kwa misingi ya uadilifu, sheria, na amani.

“Mmeapa kuwatumikia wananchi. Hakikisheni mnatekeleza yale mliyowaahidi. Ondoeni chuki, dalilieni amani na mshikamano kwa kuwa maendeleo hayapatikani bila utulivu,” alisema Mkude.

DC Mkude alikumbusha madiwani kuwa nafasi waliyopewa ni heshima kubwa na dhamana ya wananchi kuwatumainia katika kusimamia huduma muhimu na miradi ya maendeleo, huku akiongeza kuwa utekelezaji wa ilani ya chama utakuwa ni kipaumbele cha baraza jipya.

Habari Picha 4638
Habari Picha 4639
Habari Picha 4640

Uchaguzi wa Viongozi: Meya na Naibu Meya Wapata Ushindi

Katika uchaguzi uliofanyika mara baada ya uzinduzi wa baraza, aliyekuwa Meya wa Jiji la Arusha, Maxmillian Iranqhe, alibuka tena na ushindi mkubwa kwa kupata kura 33 kati ya 34. Julius Meideye alichaguliwa kuwa Naibu Meya kwa kura 31 kati ya 34. Akizungumza katika hafla hiyo, Meya Iranqhe alishukuru madiwani kwa kumwonyesha imani yao na kutangaza kuwa atasimamia kikamilifu utekelezaji wa ilani ya CCM pamoja na mipango ya maendeleo ya jiji.

“Tutaanzia pale tulipoishia. Kipaumbele chetu ni matengenezo ya barabara, usafi wa jiji na kuboresha mazingira. Tunataka Arusha iwe jiji la mfano nchini,” alisema Meya Iranqhe.

Meya alisisitiza pia umuhimu wa kuwekeza kwa vijana, akitaja kuwa jiji la Arusha linakadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya 600,000, ambapo vijana ni asilimia 60 ya wakazi wote. Alihimiza kwamba ni muhimu kuunda mazingira rafiki ya fursa za kiuchumi kwa vijana ili waweze kuchangia katika ukuaji wa jiji.

“Tuweke mazingira rafiki ya fursa za kiuchumi kwa vijana. Hawa ndiyo nguvu kazi ya jiji letu, na tukiwapa nafasi sahihi wataliinua Arusha kimaendeleo,” aliongeza Meya Iranqhe.

Wito wa Mshikamano na Uendelezaji wa Jamii

Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha, Jacob Rombo, aliwapongeza madiwani walioteuliwa na kuchaguliwa, akiwataka wawajibike kwa jamii na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa tija. Rombo alieleza kuwa wakati madiwani walipokuwa nje, Mkurugenzi wa Jiji, John Kayombo, na wakuu wa idara walihakikisha kuwa huduma kwa wananchi zinaendelea bila kuathirika.

Habari Picha 4642
Habari Picha 4643
Habari Picha 4644
Habari Picha 4645

“Mnarejea kwenye majukumu yenu wakati ambapo jiji limeendelea kufanya kazi kwa ufanisi. Endeleeni kushirikiana na watumishi wetu kwa misingi ya sheria na taratibu,” alisema Rombo.

Katika ujumla wa hotuba za viongozi, kauli kuu iliyojitokeza ni wito wa mshikamano, kuepuka migogoro, kuheshimu sheria na kuweka mbele maslahi ya wananchi kuliko siasa. Wananchi waliokuwepo walionyesha matumaini mapya, wakiwa na matarajio makubwa ya maboresho ya huduma, usimamizi madhubuti wa miradi, na kasi mpya ya maendeleo katika jiji la Arusha.

Habari Picha 4647

 

Habari Picha 4646

Wananchi wa Jiji la Arusha wana matumaini mapya na baraza hili jipya la madiwani. Wakati umefika kwa viongozi hawa kuonesha vitendo na kuleta maendeleo kwa wananchi wa jiji hili.

 

Mwisho .

Share This Article
Leave a Comment