WAZIRI MCHENGERWA AKABIDHIWA OFISI NA MHE. JENISTA MHAGAMA

Geofrey Stephen
3 Min Read

Na WAF, Dodoma

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa leo Novemba 19, 2025 amekabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama.

Tukio la makabidhiano ya ofisi limefanyika katika Ofisi za Wizara ya Afya Mtumba, Jijini Dodoma.

Waziri Mchengerwa amempongeza Mhe. Mhagama kwa utumishi wake hodari katika Wizara mbalimbali nchini ikiwemo Wizara ya Afya ambapo amefanya kazi kubwa ya kuboresha Sekta hiyo na kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya nchini.

Habari Picha 4496

“Mhe. Rais ameahidi ndani ya siku 100 atafanya mageuzi makubwa ya Sekta ya Afya nchini, nashukuru kwa hatua nzuri ambayo ulishaanza utekelezaji wake ikiwemo suala la Bima ya Afya kwa wote pamoja na mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza nchini, ambayo yanaleta athari kubwa ndani ya jamii,” amesema Waziri Mchengerwa.

Habari Picha 4497

Mhe. Mchengerwa amemtakia kila la heri Mhe. Mhagama na kuahidi kuendelea kushirikiana kwani Wizara ya Afya ni mhimili mkubwa katika usalama wa nchi, hivyo watajitahidi kuhakikisha ndoto za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zinatimia kwa kutekeleza kikamilifu yale yogte yaliyomo kwenye ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Awali akizungumza, Mhe. Mhagama amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumuamini kuongoza Wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Afya katika kipindi chote cha muhula wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Sita.

Mhe. Mhagama amempongeza Mhe. Mchengerwa kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Afya na Mhe. Dkt. Florence Samizi kuwa Naibu Waziri wa Afya huku akiwaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa maendeleo ya Sekta ya Afya ili kutimiza maono ya Mhe. Rais ya uboreshaji wa huduma za afya nchini.

“Imani ya Mhe. Rais kuwaleta katika Wizara hii siyo mchezo, nimekaa hapa kwa muda mfupi lakini nimegundua tunapozunguza usalama wa nchi yetu Tanzania hatuwezi kuiacha Wizara ya Afya, ina mchango mkubwa katika usalama wa wananchi katika Taifa letu,” amesisitiza Mhe. Mhagama.

Habari Picha 4498

Mhe. Mhagama amewataka watumishi wa afya nchini kuendelea kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na uzalendo zaidi kwa Taifa ili watanzania wapate huduma bora za afya.

Mwisho .

Share This Article
Leave a Comment