TPDC YAONGEZA KASI YA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA NCHINI.

Geofrey Stephen
3 Min Read

Na Mwandishi wetu.

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeendelea kuunga mkono Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwani Watanzania zaidi ya 3000 wameunganishiwa na mifumo ya gesi asilia ambayo ni nafuu zaidi kwa matumizi.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 18, 2025 Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Biashara ya Mafuta na Gesi asilia TPDC Mhandisi Emmanuel Gilbert wakati akizungumza katika Kipindi cha Kumekucha ITV, ikiwa ni muendelezo wa kuhamasisha kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na mkakati wa Mawasiliano. Ili kutoa fursa ya uelewa kwa watanzania.

Habari Picha 4455

“Kutokana na Mkakati wa Taifa wa nishati safi ya kupikia kuwa nyenzo muhimu ya kufanikisha malengo ya Taifa ya kuhakikisha wananchi wanapika kwa kutumia nishati safi, salama na rafiki wa mazingira, sisi kama TPDC tumeendelea kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia kwani tumewaunganishia wananchi takribani 3000 mifumo ya gesi asilia ambayo ni nafuu na inapatikana kwa uhakika katika Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara.”Ameeleza Gilbert.

“Tunapotekeleza mkakati mkubwa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia tunatekeleza pia makubaliano ya kimataifa yanayolenga kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa. dhamira ya Serikali ni asilimia 80 ya wananchi watumie nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.” Amesema Gilbert.

Sambamba na hilo ameeleza kuwa usambazaji wa gesi asilia umelenga kuwafikia wananchi wengi zaidi katika maeneo ya mijino na vijijini hata wale wenye kipato cha chini kwani amesisitiza kuwa TPDC imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa kusambaza mitungi ya gesi (LPG) katika maeneo ya vijijini ambazo zina mita za kujaza gesi kwa kilo ili kuhakikisha wananchi wa hali ya chini wanakidhi gharama za matumizi na wanatumia nishati safi ya kupikia.

Habari Picha 4456

Amesema kuwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita kutoa elimu kwa wananchi ili kuhakikisha kila mwananchi anapata uelewa juu ya faida za matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na kuhakikisha wadau mbalimbali wanashirikishwa ili kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa vifaa vya nishati kwa bei nafuu hususan maeneo ya vijijini.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kutumia nishati safi ya kupikia na kuachana na nishati isiyo safi kwani mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, unajikita katika kupunguza magonjwa katika mfumo wa upumuaji yanayotokana na moshi, kulinda misitu, na kuongeza fursa za kiuchumi kupitia uwekezaji katika teknolojia na vifaa vya nishati safi ya kupikia.

Mwisho

Share This Article
Leave a Comment