KESI YA HAKI ZA BINADAMU KUHUSU MAUDHUI MTANDAONI YASIKILIZWA MAHAKAMA YA AFRIKA MASHARIKI.

Geofrey Stephen
4 Min Read

Na Geofrey Stephen Arusha .

Kesi ya Kukandamiza Uhuru wa Maudhui Mtandaoni Yaanza Kusikilizwa Mahakama ya Afrika Mashariki

Novemba 13, 2025, Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) ilisikiliza shauri lenye uzito mkubwa linalopinga baadhi ya vifungu vya Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA), huku mashirika ya utetezi wa haki za binadamu yakidai kuwa vifungu hivyo vinakiuka haki za binadamu na Mkataba wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC).

Habari Picha 4420
Habari Picha 4421

Shauri hili namba 30/2020 limefunguliwa na mashirika manne ya haki za binadamu nchini Tanzania: Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), na Center for Strategic Litigation (CSL), dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kesi hiyo ilisikilizwa mbele ya majaji watano wa Mahakama ya Afrika Mashariki: Jaji Johanes Masara, Jaji Richard Wejuri, Jaji Richard Muhumuza, Jaji Dkt. Gacuko Leonard, na Jaji Kayembe Kasanda.

Mashirika Yadai Sheria Inaminya Uhuru wa Mawasiliano

Wakili Jeremiah Mtobesya na Peter Majanjala, waliowakilisha waleta maombi, walieleza mahakama kuwa baadhi ya vifungu vya Kanuni za Maudhui Mtandaoni — ikiwa ni pamoja na vifungu 3, 4, 5, na 6 — vina mapungufu makubwa na vinakiuka uhuru wa kujieleza na kutoa taarifa.

Mtobesya alisema, “Sheria yoyote inapaswa kuzingatia misingi ya haki za binadamu, ikiwemo uhuru wa kupokea na kutoa taarifa. Hata baada ya marekebisho ya mwaka 2022 na 2025, bado kuna vifungu vinavyokinzana na haki hizi za msingi.”

Aliongeza kuwa adhabu zilizowekwa, ikiwa ni pamoja na faini ya hadi Sh milioni 5 au kifungo cha miezi 12, ni kali kupita kiasi na zinaweza kuwatisha wananchi kutumia haki yao ya kujieleza mtandaoni.

Kwa upande mwingine, Wakili Majanjala alieleza kuwa taratibu za utoaji leseni za maudhui mtandaoni ni tata na zisizo rafiki kwa watumiaji wote, kwani si kila anayetangaza maudhui mtandaoni ni mfanyabiashara.

Habari Picha 4422

“Kanuni hizi pia zinakiuka vifungu vya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, hususan vifungu vya 6(d), 7, na 8(c), vinavyoelekeza nchi wanachama kuzingatia demokrasia, uwazi, utawala bora, na haki za binadamu,” alisisitiza Majanjala.

Serikali Yapinga Hoja, Ikisema Sheria Zipo Kwa Usalama wa Mtandao

Upande wa Serikali, uliongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Stanley Kalokola, akisaidiana na Daniel Nyakika. Wakili Kalokola alieleza kuwa marekebisho yaliyofanyika katika sheria hizo yameondoa mapungufu mengi yaliyokuwa yakilalamikiwa, na kwamba Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni hazikiuki haki za binadamu.

“Kanuni za Maudhui hazikiuki haki za binadamu. Zinatoa mwongozo wa matumizi salama ya mtandao na kulinda maslahi ya taifa bila kuvunja haki za msingi,” alisema Kalokola.

Mahakama Iahirishwa, Hukumu Itatangazwa Baadaye

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Johanes Masara aliahirisha kesi hiyo na kusema tarehe ya hukumu itatangazwa baadaye.

Shauri hili linatarajiwa kuwa na athari kubwa katika kuainisha mipaka kati ya udhibiti wa serikali mtandaoni na uhuru wa mawasiliano, na linaweza kuwa na athari muhimu kwa haki za kiraia katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

Hii ni kesi inayosubiriwa kwa hamu na wadau wa haki za binadamu, vyombo vya habari, na watumiaji wa mtandao kwa ujumla, huku kukiwa na mjadala mkubwa kuhusu usalama wa mtandao dhidi ya uhuru wa kujieleza.

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment