Na Mwandishi Wetu
MBEYA: MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Anthony Kasore, amesema taasisi hiyo imejipanga kuboresha mfumo wa mafunzo ili kuhakikisha Watanzania wanapata ujuzi unaoendana na maendeleo ya teknolojia za kisasa na mahitaji halisi ya soko la ajira.
Akizungumza alipotembelea Chuo cha VETA Mkoa wa Mbeya, Kasore alisema taasisi hiyo inaendelea kuimarisha karakana, mitambo, na vifaa vya kufundishia ili kufanikisha mafunzo ya vitendo yanayozingatia ubunifu na matumizi ya teknolojia katika sekta mbalimbali.

“Katika dunia ya sasa, mafundi wanapaswa kutumia teknolojia kugundua tatizo badala ya kutegemea uzoefu wa kusikia sauti ya injini. Ndiyo mwelekeo wa mafunzo yetu kwa sasa,” alisema Kasore.
Ameeleza kuwa VETA pia imepanua wigo wa mafunzo kwa kuanzisha kozi za sanaa za maonyesho kwa kushirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Bodi ya Filamu Tanzania, lengo likiwa ni kukuza vipaji katika maeneo ya muziki, uandaaji wa video, na utengenezaji wa tamthilia.
“Ujuzi haupo kwenye karakana pekee. Sanaa pia ni ajira na kipato, ndiyo maana tumeamua kutoa mafunzo rasmi katika eneo hili,” aliongeza.
Kuhusu makundi maalum, Kasore alisema kuwa VETA inaendelea kutoa mafunzo kwa watu wenye mahitaji maalum na wanaoishi katika mazingira magumu kupitia miradi maalum inayowafikia zaidi ya watu 1,000 kila mwaka, huku vyuo vingi vikiwa na miundombinu rafiki kwa makundi hayo.
Amefafanua pia kuwa ujenzi wa vyuo vipya 65 unaoendelea nchi nzima ni sehemu ya juhudi za serikali za kusogeza elimu ya ufundi karibu na wananchi, kwa kuzingatia mahitaji ya kiuchumi na kiteknolojia ya kila eneo.
Kasore aliongeza kuwa tarehe 17 Oktoba, VETA itakutana na waajiri na wadau wa viwanda kwa ajili ya kujadili maboresho ya mitaala na kuhakikisha mafunzo yanayoendelea yanaendana na uhalisia wa mazingira ya kazi.
“Tunataka kila mhitimu wa VETA awe na ujuzi unaotakiwa na soko. Ushirikiano wetu na waajiri ni msingi wa kuboresha ubora wa mafunzo,” alisema.
Kwa ujumla, Kasore alisisitiza kuwa dhamira ya VETA ni kumwezesha kila Mtanzania kupata ujuzi unaomwezesha kuajiriwa, kujiajiri au kuajiri wengine, ikiwa ni mchango muhimu katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.