Na Mwandishi Wetu
MBEYA: KATIBU Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, amezihimiza taasisi za dini, hususan vyuo vinavyomilikiwa au kuendeshwa na taasisi hizo, kuweka mfumo rasmi wa kutoa huduma za ushauri nasaha kwa vijana ili kuwakinga dhidi ya changamoto za msongo wa mawazo na matatizo ya afya ya akili.
Akizungumza jijini Mbeya wakati wa kufunga Kongamano la Kitaifa la Vijana, Mhandisi Zena alisema kuwa changamoto za kisaikolojia miongoni mwa vijana zimeongezeka kwa kasi kutokana na mambo mbalimbali, yakiwemo presha ya maisha, mitazamo hasi ya kijamii, na matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii.
“Taasisi za dini zina nafasi muhimu katika kujenga jamii yenye utulivu wa kisaikolojia. Vyuo vinavyosimamiwa na taasisi hizo vinapaswa kuwa na wataalamu wa ushauri nasaha watakaowasaidia vijana kupata msaada wa mapema kabla changamoto hazijazidi,” alisema.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa vijana kufanya maamuzi yenye tija katika maisha yao ya kila siku, akisema kila hatua waliyopanga kuchukua inapaswa kuzingatia maadili na matokeo yake kwa jamii.
“Kila jambo unalotenda lifikiriwe kwa makini. Maamuzi mabaya leo yanaweza kuharibu maisha yako ya baadaye. Kuwa na mizani ya maadili katika kila uamuzi,” aliongeza.
Akizungumzia hali ya afya ya akili kwa vijana, Mhandisi Zena alisema baadhi ya vijana wamejikuta wakitumia dawa za kulevya, bangi, gundi na hata dawa za usingizi kama njia ya kukabiliana na changamoto za maisha, jambo ambalo linahatarisha afya na mustakabali wao.
Alisisitiza umuhimu wa jamii kuwasaidia vijana kwa kuwapa msaada wa kihisia, kuwapa nafasi ya kueleza matatizo yao, na kuwaongoza kutafuta suluhisho kwa njia salama na kitaalamu.
Pia alitoa onyo kuhusu tabia ya vijana kutumia mitandao ya kijamii kama kipimo cha mafanikio, akieleza kuwa hali hiyo imekuwa ikichangia ongezeko la msongo wa mawazo.
“Mitandao imejaa maigizo ya maisha. Wengi wanaoonesha mafanikio siyo kweli wanamiliki wanayoyaonesha. Usiishi maisha ya mtu mwingine; tumia mitandao kujifunza na kujenga maarifa,” alisisitiza.
Katika hitimisho la hotuba yake, Mhandisi Zena alieleza kuwa kufuatilia kila siku taarifa za huzuni, migogoro au majanga kupitia vyombo vya habari na mitandao kunaweza kuongeza msongo wa mawazo bila kujua.
“Kuna watu ambao kila siku wanatafuta habari mbaya, na matokeo yake wanaishi kwenye huzuni ya kudumu. Tujifunze kuchuja aina ya taarifa tunazopokea kwa afya njema ya akili,” alihitimisha.