Elimu ya Ufundi Ni Nguzo ya Maendeleo ya Taifa – VETA

a24tv
3 Min Read

Na Mwandishi Wetu

 

MBEYA: MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesema ushiriki wake katika Maadhimisho ya Wiki ya Vijana ni hatua muhimu katika kuonesha mchango wake mkubwa katika kuwawezesha vijana kupitia elimu na mafunzo ya ufundi stadi yanayokidhi mahitaji halisi ya soko la ajira.

 

Akizungumza alipotembelea banda la VETA katika maadhimisho hayo yanayoambatana na Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore, alisema taasisi hiyo imekuwa chachu ya maendeleo kwa kutoa mafunzo yanayowawezesha vijana kugundua, kukuza, na kutumia vipaji vyao kwa maendeleo ya binafsi na ya taifa kwa ujumla.

 

Habari Picha 3506

 

“Lengo letu ni kumjengea kijana uwezo wa kutumia ujuzi alionao kujiajiri au kuajiriwa, hivyo kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa taifa,” alisema Kasore.

 

Katika maonyesho hayo, VETA imeonesha bidhaa na ubunifu mbalimbali vinavyotengenezwa na wanafunzi na wakufunzi wake, ikiwemo kazi zilizofanywa na watu wenye mahitaji maalum — jambo linaloonesha mafanikio ya utekelezaji wa elimu jumuishi inayotolewa na taasisi hiyo.

 

“Tumewasilisha bidhaa halisi na bunifu zinazotengenezwa katika vyuo vyetu ili jamii ione matokeo ya moja kwa moja ya mafunzo ya ufundi stadi tunayotoa,” aliongeza.

 

Kasore alisema pia kuwa wanawake wamekuwa sehemu muhimu ya walengwa wa programu za VETA, ambapo kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali, taasisi hiyo imetoa mafunzo yanayowawezesha wanawake kuendesha biashara na shughuli za uzalishaji kwa ufanisi zaidi.

 

“Kupitia mpango wa Wanawake na Samia, zaidi ya wanawake 15,000 nchini wamepatiwa mafunzo ya ufundi na ujasiriamali, jambo ambalo limewawezesha kuongeza kipato na kujiamini kiuchumi,” alisema.

 

Habari Picha 3504

 

Aidha, aliwahimiza wazazi na walezi wenye watoto wenye mahitaji maalum kupeleka watoto wao katika vyuo vya VETA badala ya kuwaficha nyumbani, akibainisha kuwa vyuo hivyo vina walimu na miundombinu mahsusi kwa ajili ya makundi hayo.

 

Kasore alisisitiza kuwa VETA ndiyo taasisi pekee nchini yenye mamlaka ya kuandaa na kusimamia mitaala ya mafunzo ya ufundi stadi, hivyo kuhakikisha mafunzo yote yanayotolewa yanakwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira, ndani na nje ya nchi.

 

“Tunajivunia kuwa chombo kinachounda kizazi cha vijana wabunifu, wachapakazi na wenye uwezo wa kubadilisha changamoto kuwa fursa za maendeleo,” alihitimisha.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment