Majaliwa: Serikali Yazindua Programu Maalum ya Uanagenzi Kwa Ajili ya Vijana

a24tv
3 Min Read

Na Mwandishi Wetu

 

MBEYA: Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeanzisha programu maalum ya Uanagenzi kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, inayolenga kuwapatia vijana wa Kitanzania ujuzi wa kazi bila kujali kiwango chao cha elimu, ili kuwawezesha kujitegemea kiuchumi.

 

Akizungumza katika Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayoendelea mkoani Mbeya, Majaliwa alisema mpango huo unawalenga vijana wote nchini, hususan wale wanaoishi katika mazingira magumu, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

 

“Kupitia programu hii, serikali inawalipia ada kwa miezi sita vijana wanapokuwa wakipata mafunzo vyuoni. Baada ya kuhitimu, wanakuwa na uwezo wa kujiajiri, kuanzisha vikundi vya uzalishaji mali au hata kuajiri wengine,” alisema Majaliwa.

 

Ameeleza kuwa vijana hao hupatiwa mafunzo ya stadi mbalimbali zinazochochea ajira na ukuaji wa uchumi, ikiwemo ufundi wa magari, umeme, TEHAMA, uchomeleaji, usindikaji na ufungashaji wa vyakula, ususi, urembo na ushonaji.

 

Habari Picha 3412

 

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, tangu kuanzishwa kwa programu hiyo mwaka 2022 hadi sasa, jumla ya vijana 77,228 wamepatiwa mafunzo katika vyuo mbalimbali vya elimu ya ufundi nchini.

 

Ameongeza kuwa Maadhimisho ya Wiki ya Vijana ni sehemu ya Siku ya Kimataifa ya Vijana inayotambuliwa duniani kote, yenye lengo la kutoa fursa kwa vijana kujadili mafanikio, changamoto na nafasi yao katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

 

“Tuitumie siku hii kuwasikiliza vijana wetu, wajieleze changamoto wanazokabiliana nazo, ili serikali iweze kuchukua hatua stahiki,” alisisitiza Majaliwa.

 

Aidha, alibainisha kuwa Serikali imefanya maboresho ya Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2017 na sasa inatekeleza sera mpya ya mwaka 2024, inayolenga kuboresha maisha ya vijana kwa kushirikiana nao na wadau mbalimbali wa maendeleo.

 

Pia, Serikali imeimarisha programu za uwezeshaji kiuchumi na utoaji wa elimu ya ujuzi bila malipo, huku kwa upande wa elimu ya juu ikiendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na kuboresha vyuo vya elimu ya kati na ufundi stadi ili kuwaandaa vijana kuingia kwenye soko la ajira kwa ufanisi zaidi.

 

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, alisema maadhimisho hayo ya kila mwaka ni jukwaa muhimu linalowaunganisha wadau wa maendeleo kutathmini mchango wa vijana katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii.

 

“Ni fursa ya kuwakumbuka na kuwaenzi waasisi wa taifa letu kama Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, ambao wakiwa katika umri wa ujana waliongoza harakati za ukombozi wa Afrika,” alisema Kikwete.

Share This Article
Leave a Comment