Na Geofrey Stephen Arusha .
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeweka wazi ratiba ya ujio wa mgombea mwenza wa urais, Dkt. Emmanuel Nchimbi, mkoani Arusha mnamo Septemba 12, 2025. Ziara hii inatarajiwa kuvuta umati mkubwa wa wanachama na wananchi, huku chama kikisisitiza mshikamano na hamasa kuelekea uchaguzi mkuu.
Ratiba ya Ziara ya Dkt. Nchimbi – Arusha
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa, Saipulani Remsey, Dkt. Nchimbi atapita kwenye maeneo yafuatayo:

Saa 2:00 asubuhi – Mapokezi Wilayani Longido
Saa 5:00 asubuhi – Mkutano Arumeru (Bypass)
Saa 7:00 mchana – Mkutano Mkuu Uwanja wa Soweto, Arusha
Remsey ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi, akisema mkutano wa Soweto utakuwa wa kihistoria kwani Dkt. Nchimbi atamwombea kura Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha, Paul Makonda.
Mapokezi Yenye Hamasa
Chama kimeandaa mabasi kwa ajili ya usafiri wa wafuasi kutoka maeneo mbalimbali ili kuhakikisha kila mmoja anafika kwa wakati.
“Sasa hivi tunatumia mabasi kuwabeba wafuasi wetu na siyo tena punda. Raha ya mwanasiasa ni kuona uwanja umefurika wananchi wenye hamasa,” alisema Remsey kwa msisitizo.
Zaidi ya hapo, mkutano huo utapambwa na magari yenye rangi za mabakamabaka ya kampeni za mgombea ubunge Paul Makonda. Remsey alitoa ufafanuzi kwamba hayo si magari ya JWTZ bali ni ya kampeni za chama.
Maoni ya Wananchi
Wananchi jijini Arusha wamepokea kwa shauku taarifa za ujio wa Dkt. Nchimbi.
Mwanachama mmoja jijini Arusha alisema:
“Tunatarajia kusikia mipango ya chama chetu kuendelea kuboresha maisha ya wananchi. Ujio huu unatupa matumaini makubwa ya ushindi.”
“CCM ni chama chetu na ujio huu unatuamsha zaidi. Vijana tupo tayari kushirikiana kuhakikisha ushindi wa Rais Samia na wagombea wetu unapatikana.”
Hitimisho
Kwa ujumla, ziara hii ya Dkt. Nchimbi inalenga kuimarisha kampeni za urais na ubunge katika Mkoa wa Arusha. Ni ishara ya mshikamano wa chama na hatua ya kuongeza hamasa kuelekea uchaguzi ujao.
Mwisho .