TULIA ACKSON AONGOZA MAANDALIZI YA MKUTANO MKUBWA WA IPU ARUSHA, VIONGOZI 2,000 KUTUA TANZANIA.

Geofrey Steven
2 Min Read

Na Geofrey Stephen ARUSHA, TANZANIA –

Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, ambaye pia ni Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo Oktoba 3, 2026, ameongoza kikao cha Kamati Tendaji ya IPU kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).

Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, kikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026.

Habari Picha 21650
Habari Picha 21651

Mkutano huo wa kimataifa unatarajiwa kufunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na unatarajiwa kukutanisha takribani washiriki 2,000 kutoka mabunge 183 wanachama wa IPU duniani.

Washiriki hao wanatarajiwa kujumuisha Maspika wa Mabunge, Wabunge, Makatibu wa Mabunge pamoja na maafisa mbalimbali wa mabunge kutoka mataifa tofauti duniani.

Mkutano Mkuu wa 153 wa IPU unatarajiwa kuwa jukwaa la viongozi na wawakilishi wa mabunge kujadili masuala mbalimbali yanayohusu ushirikiano wa kimataifa, demokrasia na nafasi ya mabunge katika kushughulikia changamoto zinazolikabili dunia.

Habari Picha 21653
Habari Picha 21652

Kufanyika kwa mkutano huo jijini Arusha kunaweka Tanzania katika nafasi ya kuwa mwenyeji wa viongozi na wawakilishi wa mabunge kutoka sehemu mbalimbali za dunia, huku maandalizi yakiendelea kuhakikisha mkutano huo unafanyika kwa mafanikio.

Mwisho…

Share This Article
Leave a Comment