Na Geofrey Stephen ARUSHA
JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) na Serikali ya China leo, Oktoba 5, 2026, zimesaini mkataba wa msaada wa dola 180,000 za Marekani katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya EAC jijini Arusha.
Msaada huo unalenga kusaidia shughuli za jumuiya pamoja na kujenga uwezo wa taasisi zake, huku EAC ikiiomba China kuongeza ushirikiano kwa kuelekeza zaidi fedha, teknolojia na utaalamu katika miradi ya miundombinu, biashara, nishati safi na teknolojia.


Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Stephen Mbundi, alisema msaada kutoka China umekuwa na mchango mkubwa katika shughuli za jumuiya hiyo na umefika pia katika ngazi ya wananchi.
Alisema fedha hizo zimekuwa zikisaidia shughuli mbalimbali, zikiwemo ufuatiliaji wa uchaguzi, maonesho ya biashara kwa wajasiriamali wadogo, kujenga uwezo wa watumishi pamoja na kuimarisha mawasiliano kuhusu ajenda ya ujumuishaji wa kikanda.
“Tunashukuru na kuthamini mchango huu. Msaada wa China umefika hadi ngazi ya chini kupitia kusaidia maonesho ya Jua Kali, hivyo unaonekana moja kwa moja kwa wananchi,” alisema Balozi Mbundi.
EAC YAOMBA CHINA KUONGEZA MSAADA
Pamoja na kuthamini msaada huo, Balozi Mbundi alisema EAC sasa inataka ushirikiano na China upanuliwe zaidi ili kusaidia miradi mikubwa ya maendeleo yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi wa nchi wanachama.
Alisema EAC inapendekeza China kuongeza ushirikiano katika maeneo ya miundombinu ya biashara na usafirishaji, viwanda na kuongeza thamani ya bidhaa, nishati safi, biashara ya kidijitali, usalama wa chakula, teknolojia pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, alisema EAC inahitaji China kuendelea kusaidia upatikanaji wa vifaa vya TEHAMA na kuongeza fursa za mafunzo ya kitaalamu kwa watumishi wa jumuiya hiyo.
CHINA YAHAIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA EAC.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, alisema Serikali ya China itaendelea kushirikiana na EAC katika kuimarisha ujumuishaji wa kikanda na maendeleo ya nchi wanachama.
Alisema China imetoa dola 180,000 za Marekani kwa EAC kwa ajili ya kujenga uwezo, kusaidia bajeti na kuwezesha shughuli mbalimbali za jumuiya.
“China inafurahi kutoa dola 180,000 za Marekani kwa EAC kwa ajili ya kujenga uwezo na bajeti,” alisema Balozi Chen.


Alisema China inatambua hatua ambazo EAC imepiga katika mchakato wa ujumuishaji wa kikanda na iko tayari kuendelea kushirikiana na jumuiya hiyo kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa nchi wanachama.
USHIRIKIANO SI FEDHA PEKEE.
Balozi Mbundi alisema ushirikiano kati ya EAC na China haujajikita kwenye fedha pekee, bali pia umehusisha mafunzo, kubadilishana uzoefu, uhamishaji wa maarifa na utoaji wa vifaa.
Alitoa mfano wa magari manane yaliyotolewa na Serikali ya China mwaka 2023 yenye thamani ya takribani dola 400,000 za Marekani, ambayo yamekuwa yakitumika kusaidia shughuli za EAC na baadhi ya taasisi nyingine za kikanda.
“Magari haya hayasaidii EAC pekee. Moja limepelekwa Tume ya Bonde la Ziwa Victoria na mengine yanatumika katika shughuli mbalimbali. Hata tunapokuwa na mikutano mikubwa hapa, waandaaji huja kwetu na kuyaomba kwa matumizi yao,” alisema.
EAC YATAKA MIRADI YA KIKANDA.
Balozi Mbundi alisema EAC inapendekeza kuanzishwa kwa mazungumzo maalumu kati ya jumuiya hiyo na China yatakayolenga kubaini miradi ya kikanda yenye kipaumbele na kuweka mazingira ya ushirikiano katika fedha, teknolojia, uhamishaji wa maarifa, ujenzi wa uwezo na ushiriki wa sekta binafsi.
“Tunakaribisha ushirikiano unaounganisha fedha, teknolojia, uhamishaji wa maarifa, ujenzi wa uwezo na ushiriki wa sekta binafsi,” alisema.
Alisema ushirikiano huo unapaswa kulenga miradi yenye uwezo wa kuunganisha nchi wanachama, kukuza biashara na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Afrika Mashariki.
EAC YAUNGA MKONO SERA YA “CHINA MOJA”
Aidha, Balozi Mbundi alisema EAC inaunga mkono sera ya China ya “China Moja”, akieleza kuwa jumuiya hiyo inaweza kujifunza kutoka China katika safari yake ya kuelekea kuwa shirikisho la kisiasa.
“EAC inalenga kuwa shirikisho la kisiasa, ambapo tutakuwa na kituo kimoja cha kisiasa. Kwa mantiki hiyo, tunaunga mkono sera ya China Moja kwa sababu tunaona kuna mambo yanayofanana na tuna mengi ya kujifunza kutoka China,” alisema.

Alisema vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo ya Dunia (GDI) vinaendana na Mkakati wa Saba wa Maendeleo wa EAC unaolenga kuharakisha maendeleo ya nchi wanachama.
Balozi Mbundi aliishukuru Serikali ya China kwa kuendelea kuunga mkono ajenda ya ujumuishaji wa Afrika Mashariki, akisema EAC iko tayari kuimarisha zaidi ushirikiano huo, hususan katika miradi yenye tija kwa uchumi na wananchi wa ukanda huo.
MWISHO.
