ZARAU YAWAKA: WANANCHI WAILILIA BILI KUBWA ZA MAJI

Geofrey Steven
4 Min Read

HAI, KILIMANJARO .

Baadhi ya wakazi wa Kitongoji cha Zarau, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, wamelalamikia ankara kubwa za maji wanazopokea, wakisema hazilingani na matumizi yao halisi.

Malalamiko hayo yalitolewa Septemba 29, 2026, katika mkutano wa kawaida wa Kitongoji hicho uliofanyika katika Shule ya Msingi Bomang’ombe, ambapo wananchi walijadili masuala mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo changamoto ya mgao wa maji, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha moramu na utoro wa wanafunzi shuleni.

Habari Picha 21542
Habari Picha 21543

Wananchi hao wamesema pamoja na kupata maji kwa mgao, bado wamekuwa wakipokea bili kubwa, hali ambayo imeibua maswali kuhusu usahihi wa ankara hizo, hususan kwa wananchi wenye kipato cha chini.

Mmoja wa wakazi hao, John Munisi, amesema maji katika eneo lao hupatikana takribani mara mbili kwa wiki, hali ambayo haiwatoshi kwa matumizi ya kawaida na kuwalazimu kutumia muda mwingi kutafuta maji katika maeneo mengine.

Amesema wakati mwingine maji hutoka mara mbili au tatu kwa wiki, lakini wananchi hawapati taarifa sahihi kuhusu ratiba ya mgao huo.

“Maji yanaweza kutoka mara mbili au tatu kwa wiki, lakini hatujui kama ni mgao au kuna tatizo gani kwa sababu hatupewi taarifa,” amesema Munisi.

Kwa upande wake, Mariamu Ibrahimu amesema ankara anazopokea hazilingani na kiasi cha maji anachotumia.

Amesema awali alikuwa akilipa takribani Shilingi 4,000 kwa mwezi, lakini tangu mwanzoni mwa mwaka huu amekuwa akilipia hadi Shilingi 10,000, licha ya matumizi yake ya maji kuwa madogo.

“Natumia maji kidogo lakini ninapokea bili kubwa. Hilo linanifanya niwe na wasiwasi kuhusu uhalali wa bili ninazotozwa,” amesema Ibrahimu.

Mwenyekiti awataka wananchi kushirikishwa katika usomaji wa mita

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Zarau, Michael Mshana, amewataka mafundi wanaohusika na usomaji wa mita za maji kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna mita zinavyosomwa ili kupunguza malalamiko kuhusu bili.

Mshana pia ameshauri mafundi kuwashirikisha wananchi wakati wa kusoma mita majumbani, akisema hatua hiyo inaweza kusaidia kuongeza uwazi na kuondoa malalamiko ya baadhi ya wateja kuhisi kuwa wanatozwa bili zisizoendana na matumizi yao.

Utoro wa wanafunzi nao wazungumziwa

Katika mkutano huo, wananchi pia walijadili changamoto ya utoro wa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari zilizopo katika maeneo hayo.

Waliahidi kushirikiana na uongozi wa Kata kuhakikisha tatizo hilo linapungua.

Mshana amesema Serikali, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya ujenzi na kuboresha miundombinu ya shule, hivyo jamii inapaswa kuhakikisha watoto wanatumia fursa hizo kupata elimu badala ya kuacha utoro ukiendelea.

Bodi ya Maji yaeleza kuhusu bili na mgao

Akizungumza kwa njia ya simu kuhusu malalamiko ya bili, Meneja wa Bodi ya Maji Losaa, Jerry Joseph Kia, amewataka wateja kutoa ushirikiano pale wanapobaini changamoto katika ankara zao.

Amesema mteja anapopokea ujumbe mfupi wa simu unaohusu bili au malipo ya maji, anapaswa kuhakiki taarifa hizo na kutoa taarifa kwa Bodi endapo atabaini tatizo.

Kia amesema namba za mawasiliano zipo kwa ajili ya wateja kutoa taarifa na kwamba ushirikiano kati ya wananchi na Bodi ni muhimu katika kutatua changamoto hizo.

 

Habari Picha 21541

Kuhusu mgao wa maji, amesema changamoto hiyo ipo katika eneo hilo kutokana na upungufu wa maji katika vyanzo, lakini hatua zinaendelea kuchukuliwa ili kutatua tatizo hilo na kuondoa adha kwa wananchi.

Mwisho..

Share This Article
Leave a Comment