Moshi.
Waislamu nchini wametakiwa kujiandikisha mapema na kulipia gharama za huduma za mahujaji ili kuwezesha maandalizi ya ibada ya Hijja kufanyika kwa wakati.
Mwisho wa kujiandikisha na kukamilisha malipo kwa ajili ya ibada hiyo ni Septemba 26, 2026, kwa mujibu wa utaratibu mpya uliowekwa kwa ajili ya maandalizi ya mahujaji kutoka Tanzania.
Rai hiyo imetolewa katika Kongamano la Hijja lililofanyika katika Msikiti wa Riadha, Manispaa ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, lililowakutanisha Waislamu na Masheikh kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo kwa lengo la kutoa elimu kuhusu utaratibu mpya wa utekelezaji wa ibada ya Hijja.

Akizungumza katika kongamano hilo, Afisa wa Uratibu wa Hijja Tanzania Bara, Twahir Musawa, amesema utaratibu wa kujiandikisha na kulipia gharama za Hijja mapema utasaidia kuboresha maandalizi na huduma kwa mahujaji.
Musawa amesema hapo awali waumini wengi walikuwa wakijitokeza kwa wingi katika kipindi cha mwezi wa Ramadhani, hali iliyosababisha baadhi yao kukosa nafasi na taasisi husika kushindwa kufanya maandalizi muhimu kwa wakati.
“Ni kweli utaratibu wa zamani watu walikuwa wanajitokeza kipindi cha mwezi wa Ramadhani kwa wingi sana mpaka watu wanakosa nafasi, taasisi zinashindwa kufanya matayarisho muhimu na hata kusababisha mlipaji kushindwa kusafiri kutimiza ibada hiyo kwa mwaka husika,” amesema Musawa.

Amesema kutokana na changamoto hizo, Wizara ya Hijja ya Serikali ya Saudi Arabia imeweka utaratibu unaolenga kuhakikisha Tanzania inaendana na nchi nyingine katika maandalizi ya ibada hiyo.
Musawa amesisitiza umuhimu wa Waislamu kukamilisha malipo kabla ya tarehe Septemba 26, 2026, ili maandalizi yote muhimu yaweze kufanyika mapema.
Amesema, “Kama mambo ya dunia yamewekewa utaratibu wa muda mrefu sana, kwa nini ibada yetu ya Hijja mambo yaende hovyo bila utaratibu mzuri? Na sisi lazima tuweke utaratibu mzuri.”
Kwa upande mwingine, Musawa amesema mpango huo unalenga pia kuwezesha mamlaka kujua mapema idadi ya mahujaji kutoka Tanzania wanaotarajiwa kwenda Saudi Arabia kwa ajili ya ibada hiyo.
Ameeleza kuwa Serikali ya Saudi Arabia imeitengea Tanzania nafasi ya mahujaji zaidi ya 25,000, huku idadi ya mahujaji kutoka Tanzania mwaka jana ikiwa takribani 4,400 pekee.
Amesema Wizara ya Hijja ya Saudi Arabia imewataka waandaaji wa Hijja kuhakikisha taratibu zote pamoja na huduma muhimu zinakamilishwa na kulipiwa mapema kabla ya mahujaji kuwasili nchini humo, ili watakapofika wawe tayari kwa ajili ya kutekeleza ibada.
MAKONGAMANO YATOA ELIMU KWA WAISLAMU
Akizungumza katika kongamano hilo, Katibu wa Mufti, Sheikh Musa Hemed, amesema makongamano hayo yamekuwa yakifanyika tangu mwaka 2023 na yameendelea kutoa matokeo chanya katika kuwafikia Waislamu wanaotaka kutekeleza ibada ya Hijja lakini hawajui taratibu za kuanza.
Hemed amesema bado kuna Waislamu wenye uwezo wa kifedha wa kutekeleza ibada hiyo lakini hawana taarifa sahihi kuhusu hatua wanazopaswa kuchukua.
Amesema idadi ya Waislamu wanaopata elimu kupitia makongamano hayo imekuwa ikiongezeka kila mwaka, huku akieleza kuwa takribani watu 200 hadi 300 wamekuwa wakinufaika katika maeneo mbalimbali.
“Makongamano haya yameleta tija kubwa sana. Kuna Waislamu wana uwezo na wana fedha zao lakini hawajui wataanza vipi kutekeleza ibada hiyo,” amesema Hemed.
Amesema Tanzania bado haijatumia kikamilifu nafasi ya zaidi ya mahujaji 25,000 iliyopewa na Serikali ya Saudi Arabia, akitolea mfano nchi kama Indonesia, Malaysia na Nigeria ambazo hupeleka idadi kubwa zaidi ya mahujaji.
Hemed amesema makongamano hayo yataendelea kufanyika ili kuongeza uelewa na idadi ya Watanzania wanaotekeleza ibada ya Hijja, huku akiwataka Masheikh, Maimamu na viongozi wa misikiti kuendelea kutoa elimu hiyo kwa Waislamu katika maeneo yao.
BAKWATA KILIMANJARO YAUNGA MKONO
Kwa upande wake, Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Kilimanjaro, Awazi Lema, ameshukuru kwa kufanyika kwa kongamano hilo katika mkoa huo, akisema limewapa Waislamu fursa ya kupata elimu muhimu kuhusu ibada ya Hijja.
Lema ameahidi kushirikiana na viongozi wa Wilaya pamoja na viongozi wa misikiti kuhakikisha elimu hiyo inaendelea kuwafikia Waislamu wengi zaidi katika mkoa huo.
Mwisho.
