RAIS DKT. SAMIA AFUNGUA MKUTANO MKUU WA MWAKA WA CHAMA CHA MAWAKILI WA SERIKALI TANZANIA (TPBA) JIJINI ARUSHA.

Geofrey Steven
3 Min Read

Na Geofrey Stephen .

Arusha, Julai 13, 2026 –

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amefungua rasmi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), ukiwakutanisha mawakili wa Serikali, viongozi wa taasisi mbalimbali na wadau wa sekta ya sheria kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Habari Picha 19271

Mkutano huo ni jukwaa muhimu la kujadili maendeleo ya taaluma ya sheria, kuimarisha ushirikiano miongoni mwa mawakili wa Serikali na kuweka mikakati ya kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za kisheria kwa maslahi ya Taifa.

Habari Picha 19270

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Rais Dkt. Samia alieleza umuhimu wa kuendelea kuimarisha utawala wa sheria, uwajibikaji na maadili ya utumishi wa umma. Alisisitiza kuwa mawakili wa Serikali wana nafasi kubwa katika kulinda maslahi ya Taifa, kuhakikisha sheria zinatekelezwa ipasavyo na kuimarisha imani ya wananchi kwa mfumo wa haki.

Kabla ya kufungua rasmi mkutano huo, Rais Dkt. Samia alipokea nakala ya kitabu kiitwacho Mama Samia Doctrine of Law (Falsafa ya Sheria ya Mama Samia), kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari. Kitabu hicho kinaelezea falsafa ya uongozi wa Rais Samia, historia yake pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha utawala wa sheria, mageuzi ya taasisi za umma na maendeleo ya Taifa.

Habari Picha 19272
Habari Picha 19273

Katika hafla hiyo, Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) kilimtunuku Rais Dkt. Samia Tuzo ya Heshima kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha sekta ya sheria, utawala wa sheria na utoaji wa haki nchini. Tuzo hiyo ilikabidhiwa na Rais wa TPBA, Bw. Bavoo Anatoly Junus, mbele ya washiriki wa mkutano huo.

Kabla ya hafla ya ufunguzi, Rais Dkt. Samia pia alitembelea mabanda mbalimbali ya maonesho yaliyokuwa yakionesha kazi na huduma zinazotolewa na taasisi za sekta ya sheria. Maonesho hayo yalitoa fursa ya kuonesha mafanikio, ubunifu na hatua mbalimbali zinazochukuliwa katika kuboresha huduma za kisheria nchini.

Habari Picha 19275
Habari Picha 19274

Mkutano Mkuu wa TPBA wa mwaka huu unatarajiwa kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya taaluma ya sheria, matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za kisheria, kuimarisha uwezo wa mawakili wa Serikali pamoja na kubadilishana uzoefu kuhusu changamoto na fursa zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao.

Habari Picha 19276

Kupitia mkutano huu, Serikali inaendelea kuonesha dhamira yake ya kujenga taasisi imara za haki, kuimarisha utawala wa sheria na kuhakikisha kuwa sekta ya sheria inaendelea kuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya Taifa.

 

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment