Na Richard Mrusha A24TV
Sekta ya utalii nchini Tanzania imeendelea kushuhudia ukuaji mkubwa kwa kuongeza idadi ya watalii wa kimataifa kutoka 708,000 mwaka 2021/2022 hadi kufikia 1,559,441 mwaka 2025/2026, huku mapato yakiongezeka kutoka Sh bilioni 1.74 hadi Sh bilioni 2.53, mafanikio yanayotajwa kuchochea ukuaji wa uchumi, ajira na fursa za biashara nchini.
Akizungumza na Wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana G. Mwishawa,mafanikio ya ongezeko hilo yametokana na juhudi za serikali na wadau wa sekta hiyo katika kuboresha miundombinu, huduma za utalii na kuitangaza Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Amesema katika kipindi hicho idadi ya watalii imekuwa ikiongezeka kwa wastani wa asilimia 24 kwa mwaka, hali inayoonesha kuongezeka kwa mvuto wa Tanzania kama moja ya maeneo muhimu ya utalii barani Afrika.
Mwishawa amesema mafanikio hayo yamechangiwa na maboresho ya miundombinu ya usafiri na huduma ndani na nje ya hifadhi za taifa, ikiwemo barabara, viwanja vya ndege, maeneo ya mapokezi ya wageni pamoja na kuongezeka kwa huduma za malazi zenye viwango vinavyokidhi mahitaji ya watalii.
Ameeleza kuwa kampeni ya kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia filamu ya The Royal Tour, iliyoshirikisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, imechangia kuongeza utambulisho wa vivutio vya nchi na kuvutia wageni kutoka mataifa mbalimbali.
Aidha, amesema upanuzi wa wigo wa shughuli za utalii kupitia mikutano ya kimataifa, mashindano ya riadha, marathon, gofu na shughuli nyingine za michezo umefungua milango mipya ya kuwavutia wageni ambao mbali na kushiriki shughuli hizo hupata nafasi ya kutembelea vivutio vya utalii.
Ameongeza kuwa kuimarishwa kwa utalii wa aina maalumu, ikiwemo utalii wa farasi, uvuvi wa michezo na maeneo ya maji moto, kumeongeza chaguo kwa watalii na kupanua fursa za mapato katika sekta hiyo.
Kwa mujibu wa Mwishawa, ukuaji wa utalii una manufaa mapana kwa taifa kutokana na kuchochea ajira, kuongeza kipato kwa wananchi na kufungua fursa za biashara kwa wajasiriamali wanaotoa huduma mbalimbali zinazohusiana na utalii.


Amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha huduma, kutunza rasilimali za utalii na kushirikisha wananchi katika shughuli za kiuchumi zinazotokana na sekta hiyo ili kuhakikisha ukuaji huo unakuwa endelevu na wenye manufaa kwa taifa.
Mwisho..
