AFCON 2027: BUNGE LARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA BARABARA ARUSHA, LATAKA UBORA KUZINGATIWA.

Geofrey Steven
4 Min Read

Na Geofrey Stephen

ARUSHA:

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi na upanuzi wa barabara jijini Arusha inayohusishwa na maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), huku ikisisitiza umuhimu wa kukamilisha miradi hiyo kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora.

Akizungumza Oktoba 24, 2026, jijini Arusha, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya miradi hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Aboubakar Asenga, ameipongeza Wizara ya Ujenzi pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa hatua zilizofikiwa.

Habari Picha 21925
Habari Picha 21926

Hata hivyo, amesisitiza kuwa kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo inapaswa kuendana na ubora wa kazi ili kuhakikisha barabara hizo zinakuwa imara na zenye manufaa ya kudumu kwa wananchi hata baada ya kumalizika kwa michuano ya AFCON.

Asenga amewataka wasimamizi wa miradi kuhakikisha kazi zinakamilika ndani ya muda uliopangwa bila kuathiri viwango vya ubora vilivyowekwa.

“Hakikisheni barabara hizi zinakamilika kwa ubora na kwa wakati. Barabara hizi ni mali ya Watanzania hata baada ya mashindano ya AFCON, hivyo ubora wa kazi unapaswa kupewa kipaumbele sambamba na kasi ya utekelezaji,” amesema Asenga.

Habari Picha 21928
Habari Picha 21929

Kamati yataka usimamizi kuimarishwa

Aidha, Kamati imeielekeza Wizara ya Ujenzi, viongozi wa Serikali za Mikoa na Wilaya pamoja na wasimamizi wa miradi hiyo kuimarisha ufuatiliaji ili kuhakikisha utekelezaji unazingatia masharti ya mikataba na viwango vya ubora vilivyokubaliwa.

Kamati pia imesisitiza umuhimu wa kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wanaoishi katika maeneo yanayopitiwa na miradi hiyo, ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza wakati wa ujenzi.

Serikali yatajipanga kukamilisha miradi kwa wakati

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha miradi ya barabara inayohusishwa na maandalizi ya AFCON inakamilika kwa wakati ili kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji jijini Arusha.

Amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kupunguza msongamano wa magari, kurahisisha usafiri na kuboresha mandhari ya jiji, ambalo linatarajiwa kupokea wageni mbalimbali wakati wa michuano hiyo.

Kasekenya amezitaja barabara zinazotekelezwa kuwa ni barabara kutoka katikati ya jiji la Arusha kuelekea Uwanja wa Ndege wa Arusha na kuendelea hadi Kisongo, yenye urefu wa kilomita 9.1, ambayo inapanuliwa kuwa na njia nne.

Mradi mwingine ni ujenzi wa barabara ya Mbauda/Tanganyika Packers hadi Losinyai, yenye urefu wa kilomita 70.

Habari Picha 21930
Habari Picha 21931

Amesema Serikali itaendelea kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha kazi zinafanyika kwa kasi inayotakiwa na kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa, huku maeneo ya kimkakati ya barabara hizo yakilengwa kukamilika kabla ya Machi 2027.

Wananchi wahimizwa kupendezesha jiji la Arusha

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri amewahimiza wakazi wa Arusha kushiriki katika maandalizi ya kupokea wageni kwa kuboresha mandhari ya jiji, ikiwemo kupendezesha nyumba na maeneo yanayowazunguka.

Amesema maandalizi ya AFCON hayapaswi kuishia katika ujenzi wa miundombinu pekee, bali yanapaswa kuhusisha pia ushiriki wa wananchi katika kuhakikisha jiji linakuwa safi, lenye kuvutia na linalotoa taswira nzuri kwa wageni.

Aidha, amesisitiza kuwa usimamizi wa miradi utaendelea kuimarishwa ili kuhakikisha ubora wa kazi unaendana na thamani ya fedha zinazotumika.

Miradi hiyo kuimarisha uchumi na utalii

Utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kuwa na manufaa ya muda mrefu kwa jiji la Arusha na Mkoa wa Arusha kwa ujumla, ikiwemo kuboresha mtiririko wa magari, kurahisisha usafiri na usafirishaji, kuchochea shughuli za kiuchumi na kuongeza fursa za ajira.

Vilevile, kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara kunatarajiwa kuimarisha sekta ya utalii kwa kurahisisha ufikikaji wa maeneo mbalimbali na kuongeza mvuto wa jiji kwa wageni wa ndani na nje ya nchi.

Habari Picha 21932
Habari Picha 21933
Habari Picha 21934

Hivyo, kukamilika kwa miradi hiyo kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora kutakuwa hatua muhimu katika kuboresha huduma za usafiri na kuhakikisha miundombinu inayojengwa inawanufaisha Watanzania kwa muda mrefu, hata baada ya michuano ya AFCON kumalizika.

Mwisho…

Share This Article
Leave a Comment