Na Mwanshi wetu wa A24tv.
Idadi ya Watanzania wanaonufaika na huduma za bima nchini imefikia Milioni 26.8, ikiwa ni ongezeko la Watanzania Milioni moja ndani ya mwaka mmoja.
Hayo yamebainishwa jana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) wakati wa uzinduzi rasmi wa Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima kwa mwaka 2025, uliofanyika Oktoba 16, 2026 Jijini Dodoma.
Akizindua taarifa hiyo, Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware, alisema idadi hiyo imeongezeka kutoka Milioni 25.9 mwaka 2024 hadi Milioni 26.8 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 3.5.

Alibainisha kuwa kati ya wanufaika hao, wakata bima wenyewe ni Milioni 8.7 huku wanufaika wengine kupitia familia na makundi ni Milioni 18.1.
“Hii ni hatua kubwa. Ina maana kuwa karibu nusu ya Watanzania sasa wameingia kwenye mfumo rasmi wa ulinzi wa bima, jambo ambalo linaimarisha ustawi wa jamii na uchumi wa Taifa,” alisema Dkt. Saqware.
Pamoja na ongezeko la wanufaika, Dkt. Saqware alisema sekta ya bima imekua kwa kasi katika mtaji na uwekezaji.
Amesema mtaji halisi wa sekta hiyo umeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 697.4 mwaka 2024 hadi Shilingi Trilioni 1.89 mwaka 2025, huku uwekezaji ukiongezeka kutoka Trilioni 1.41 hadi Trilioni 2.24.
“Mali za sekta ya bima zimeongezeka kutoka Trilioni 2.14 hadi Trilioni 4.06, wakati ada za bima zilizoandikishwa zimeongezeka kutoka Trilioni 1.52 hadi Trilioni 2.55,” alisema.

Aliongeza kuwa ajira rasmi sekta ndogo ya bima zimeongezeka kwa asilimia 139.3, kutoka ajira 6,434 mwaka 2024 hadi ajira 15,398 mwaka 2025.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bima za kawaida zimekua kwa asilimia 44, bima za afya kwa asilimia 38.6 na bima za maisha kwa asilimia 14.
Dkt. Saqware alisema TIRA inalenga kukamilisha Sera ya Taifa ya Bima na kuboresha sheria na kanuni ili sekta hiyo iendane na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Naye Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mshamu Ali Munde, ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliipongeza TIRA na kusema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ili Watanzania wengi zaidi waingie kwenye bima.

“Tunataka kila Mtanzania awe na bima. Serikali itashirikiana na wadau wote kupanua wigo wa huduma hizi,” alisema Mhe. Munde.
Mwisho..
