SUMA: SIFA GOSPEL ARUSHA TUTASIFU, TUTAABUDU NA KULIOMBEA TAIFA

Geofrey Steven
4 Min Read

Na Geofrey Stephen Arusha .

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Ibada kubwa ya kusifu na kuabudu ya Sifa Gospel Fest 2026, Suma Mwaitenda, amesema maandalizi ya ibada hiyo jijini Arusha yamekamilika, huku akisisitiza kuwa wakazi wa Arusha watapata fursa ya kusifu, kuabudu na kuliombea Taifa kwa amani, umoja na mshikamano.

 

Madam Suma amesema Arusha inakuwa mkoa wa nne kufikiwa na Sifa Gospel Fest 2026, baada ya kufanyika kwa mafanikio katika mikoa ya Mbeya, Geita na Mwanza.

Habari Picha 21690
Habari Picha 21691

 

Akizungumza kuhusu maandalizi ya ibada hiyo, Suma amesema:

 

“Arusha ni mkoa wetu wa nne. Tulianza Mbeya, tukaenda Geita, Mwanza na sasa tupo Arusha. Hii ni fursa kubwa kwa wakazi wa Arusha, waumini na hata wale ambao si waumini, wote wanakaribishwa kwenye ibada hii.”

 

Amesema ibada hiyo itafanyika Jumamosi, Oktoba 10, 2026, katika Viwanja vya Shule ya Sinoni, kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa 4:00 usiku.

 

Kwa mujibu wa Suma, moja ya malengo makuu ya Sifa Gospel Fest ni kufikisha ujumbe wa Injili kupitia uimbaji, sambamba na kuupa muziki wa Injili nafasi na thamani inayostahili.

 

“Lengo kuu la ibada hii ni kufikisha Injili kupitia uimbaji, na kuupa thamani muziki wa Injili ambao kwa muda mrefu umekosa jukwaa kubwa kama ambavyo aina nyingine za muziki zimekuwa zikipata heshima.”

 

KULIOMBEA TAIFA KWA AMANI NA MSHIKAMANO

 

Suma amesema mbali na kusifu na kuabudu, Sifa Gospel Fest Arusha itakuwa pia sehemu ya kuliombea Taifa la Tanzania, hasa kwa ajili ya amani, umoja, upendo, mshikamano na utulivu.

 

Amesema waumini na wananchi kwa ujumla watapata nafasi ya kuungana katika maombi, wakiliweka Taifa mbele za Mungu na kuombea Tanzania iendelee kuwa nchi yenye amani, utulivu na mshikamano miongoni mwa wananchi wake.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Habari Picha 21692

 

“Tunataka Arusha isiwe tu mahali pa kuimba na kusifu, bali iwe mahali ambapo tutasimama pamoja kuliombea Taifa letu. Tutamuomba Mungu alilinde Taifa letu, atupe amani, umoja, upendo na mshikamano, na Tanzania iendelee kuwa Taifa lenye utulivu na baraka.”

 

*SIFA YOUTH TALK*

 

Suma pia amesema kuelekea ibada hiyo, siku ya Ijumaa, Oktoba 9, 2026, kutakuwa na tukio la Sifa Youth Talk, ambalo ni kliniki maalum inayolenga kuzungumza na vijana na kuwaongezea thamani katika sekta mbalimbali.

 

Amesema mada zitahusu maeneo mbalimbali ikiwemo uchumi, vipaji, jamii pamoja na afya ya akili.

 

Tukio hilo litafanyika katika Hoteli ya Lush Garden, kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana.

 

WASANII NA WATUMISHI WA MUNGU KUTOA HUDUMA

 

Katika ibada hiyo, watumishi wa Mungu na waimbaji wakubwa wa muziki wa Injili wanatarajiwa kushiriki katika kuhubiri, kusifu na kuabudu.

 

Miongoni mwa watakaokuwepo ni Rose Muhando, Paul Clement, Christina Shusho, Upendo Nkone na Henrick Mruma, pamoja na waimbaji na kwaya mbalimbali.

Habari Picha 21693
Habari Picha 21694
Habari Picha 21695
Habari Picha 21696

Sifa Gospel Fest 2026 Arusha — Tutasifu, Tutaabudu na Kuliombea Taifa.

 

Mwisho…

Share This Article
Leave a Comment