SIHA, KILIMANJARO —
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Aggrey Mwanri, amekemea vikali vitendo vya ukabila na udini, akisema vinaweza kuhatarisha umoja, mshikamano na amani iliyopo miongoni mwa wananchi wa Wilaya ya Siha na Tanzania kwa ujumla.
Mwanri alitoa kauli hiyo Septemba 23, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya CCM Sanya Juu, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro..

Katika mkutano huo, Mwanri aliwataka wananchi kuendelea kulinda umoja na mshikamano, akisisitiza kuwa tofauti za kikabila au kidini hazipaswi kutumiwa kama chombo cha kuwagawa wananchi.
Alisema baadhi ya watu wanapokosa hoja huamua kutumia masuala ya ukabila na udini kuwagawa wananchi, hivyo akawataka wakazi wa Siha kutokubali kuchochewa na vitendo vya aina hiyo.
“Mwaka 1995, Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere alikemea kwa nguvu zake zote chembechembe za udini na ukabila. Na hapa na mimi ninaendelea kuzikemea; hatutaki kuzisikia zikiendelea,” alisema Mwanri.

Aliongeza kuwa Siha imejijengea utamaduni wa kuwathamini watu kwa kuzingatia uwezo wao na mchango wao katika jamii, badala ya kuangalia kabila au eneo wanakotoka.
“Msianze kuangaliana kwa makabila hapa. Hakuna sumu mbaya kama kuleta ukabila. Mkimuona mtu anaendekeza tabia za namna hiyo, mzomeeni,” alisema.
Mwanri pia alionya kuwa chokochoko zinazolenga kuchochea chuki za kikabila au kidini zikipewa nafasi zinaweza kuwa na madhara makubwa kwa mshikamano wa jamii na Taifa kwa ujumla.
Mwanri Akemea Rushwa Uchaguzi wa Ndani wa CCM.
Katika hatua nyingine, Mwanri alikemea vitendo vya rushwa na utoaji wa hongo kwa wananchi kwa lengo la kutafuta uungwaji mkono katika uchaguzi wa ndani wa CCM unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Alisisitiza kuwa mchakato huo unapaswa kuendeshwa kwa kuzingatia taratibu, kanuni na misingi ya chama.


Boisafi Atoa Wito wa Kulinda Miradi ya Serikali
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, aliwataka wananchi kuwa walinzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
Boisafi alisema wananchi wanapaswa kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kwamba miradi inatekelezwa kwa kuzingatia thamani inayostahili.
Mkoa Wataja Fedha za Miradi ya Maendeleo
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuupatia mkoa huo fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Babu alisema Serikali imetoa zaidi ya Shilingi bilioni 14 kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika Taasisi ya Magonjwa ya Kuambukiza Tanzania (TIDI).
Aidha, alisema Serikali imetoa Shilingi bilioni 6 kwa ajili ya ujenzi wa shule maalumu ya wasichana ya Kilimanjaro Girls, yenye lengo la kuibua na kukuza vipaji vya wanafunzi.


Kwa ujumla, mkutano huo ulijikita katika masuala ya kudumisha umoja na mshikamano wa wananchi, pamoja na kusisitiza umuhimu wa uadilifu katika michakato ya ndani ya chama na usimamizi wa miradi ya maendeleo.
Mwisho…
