Na Geofrey Stephen ARUSHA:
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amesema uwekezaji katika miundombinu, matumizi ya teknolojia na ubunifu ni muhimu katika kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza ufanisi wa mnyororo wa ugavi nchini.
Mhe. Kihenzile ameyasema hayo jijini Arusha alipomwakilisha Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, katika Mkutano wa Nane wa Afrika wa Usimamizi wa Uendeshaji na Mnyororo wa Ugavi (ACOSCM 2026), unaofanyika kwa siku mbili.

Mkutano huo umewakutanisha wataalamu, wanataaluma, watafiti na wadau wa sekta ya usafirishaji kutoka Tanzania, nchi mbalimbali za Afrika na mabara mengine.
Kupunguza gharama kunaongeza faida
Akizungumza katika kongamano hilo, Mhe. Kihenzile amesema gharama za usafirishaji ni sehemu muhimu ya gharama zinazobebwa na wazalishaji na wafanyabiashara.


Amesema wakulima, wavuvi, wafugaji, wamiliki wa hoteli na wajasiriamali wanahitaji mfumo wa usafirishaji wenye ufanisi ili bidhaa na huduma zao ziwafikie walaji na masoko kwa wakati na kwa gharama nafuu.
“Unapoweza kupunguza gharama za usafirishaji, unaongeza uhakika wa faida,” amesema.
Amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya usafirishaji kwa kujenga na kukarabati barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege, hatua zinazolenga kurahisisha usafirishaji wa watu na mizigo.


Profesa Hawa: Teknolojia itumike kutatua changamoto.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Hawa Tundui, amesema mjadala mkubwa katika kongamano hilo umejikita katika namna ubunifu na teknolojia zinavyoweza kutumika kupunguza gharama na kuongeza ufanisi katika usafirishaji, ununuzi na mnyororo wa ugavi.
Amesema teknolojia zina uwezo mkubwa wa kuboresha mifumo ya usafirishaji na ugavi, lakini matumizi yake yanapaswa kuzingatia changamoto na athari zinazoweza kujitokeza iwapo hazitatumika kwa usahihi.



“Teknolojia zina mambo mazuri sana, lakini pia zina athari zake kama hazitumiki vizuri. Tunajua kabisa kwamba zikitumika vizuri zinaweza kuboresha ufanisi,” amesema.
Kwa upande wake, Profesa Hawa amesema ni muhimu tafiti zinazofanywa na wanataaluma zisitumike katika maeneo ya kitaaluma pekee, bali zitumike kutoa ushauri na mapendekezo yatakayosaidia Serikali kutengeneza sera, miongozo na mikakati yenye manufaa kwa jamii.
“Tunaangalia ni namna gani tunaweza kuwa na mchango katika kuzisaidia Serikali zetu kupunguza gharama na kufanya kwa ufanisi zaidi kwenye masuala ya usafirishaji,” amesema.
Amesema moja ya matarajio ya kongamano hilo ni kupata mapendekezo, makubaliano au maazimio yatakayoelekeza matumizi bora ya teknolojia katika sekta za usafirishaji na mnyororo wa ugavi.
Wataalamu kutoka Afrika na mabara mengine wakutana Arusha.
Kongamano hilo limewakutanisha washiriki kutoka Tanzania, nchi za Afrika Mashariki na mataifa mengine barani Afrika, pamoja na wawakilishi kutoka Ulaya na Asia.
Miongoni mwa nchi zilizowakilishwa ni Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Nigeria, Ghana na Ethiopia.



Washiriki wanajadili uzoefu, maarifa na matokeo ya tafiti yanayoweza kusaidia kuboresha ufanisi katika sekta ya usafirishaji, ununuzi na mnyororo wa ugavi.
Profesa Hawa amesema matokeo ya mijadala hiyo yanaweza pia kusaidia watafiti kuelekeza tafiti zao katika kutatua changamoto halisi zinazozikabili Serikali na sekta mbalimbali.
Amewashukuru washiriki wote waliohudhuria kongamano hilo pamoja na Pune Foundation, shirika lisilo la kiserikali lililosaidia kufanikisha kongamano hilo.
Kongamano hilo limejikita katika kutafuta suluhisho za changamoto zinazokabili sekta ya usafirishaji na mnyororo wa ugavi, huku likisisitiza umuhimu wa kuunganisha Serikali, watafiti, wanataaluma na sekta binafsi.
Matarajio ni kupata mapendekezo na mikakati itakayosaidia kutumia teknolojia na ubunifu kuboresha ufanisi, kupunguza gharama na kuongeza manufaa ya miundombinu ya usafirishaji kwa wananchi na uchumi wa Tanzania.
MWISHO
