MAFUNZO YA ITIFAKI YAWAONGEZEA UWELEDI WANA SHERIA NA WATENDAJI WA SERIKALI ARUSHA.

Geofrey Steven
5 Min Read

Na Geofrey Stephen – Arusha.

Mtaalamu wa masuala ya itifaki, Assah Mambene, ametoa mafunzo kwa wanasheria wa serikali wanaounda Utatu wa Mkoa wa Arusha, kuhusu umuhimu wa kuzingatia taratibu, kanuni na weledi wa itifaki katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mafunzo hayo yamewalenga watendaji wanaokutana na viongozi, taasisi mbalimbali za serikali pamoja na wananchi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Habari Picha 21255

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mambene amesema itifaki ina nafasi muhimu katika kuhakikisha viongozi wanahudumiwa kwa kuzingatia hadhi na nafasi zao, huku akisisitiza kuwa kutokuzingatia taratibu za itifaki kunaweza kuathiri mahusiano na kusababisha changamoto katika shughuli za kikazi na kidiplomasia.

Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea washiriki uelewa kuhusu namna ya kuwaheshimu viongozi, kuwasiliana nao kwa staha na kufuata taratibu mbalimbali katika utoaji wa huduma za serikali.

Habari Picha 21259
Habari Picha 21260

Pallangyo: Itifaki ni muhimu katika utekelezaji wa majukumu

Kwa upande wake, James Pallangyo, Wakili wa Serikali na Mwendesha Mashtaka Kiongozi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Arusha, amesema mafunzo hayo ni muhimu kutokana na aina ya majukumu yanayotekelezwa na watendaji hao, ambao hushirikiana na wananchi pamoja na taasisi mbalimbali za serikali.

Amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka hushirikiana na taasisi nyingine katika mnyororo wa haki jinai, ikiwemo Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na TAKUKURU.

Habari Picha 21256

“Tumewaalika watu wanaohusiana na masuala ya itifaki kwa ajili ya kuwafundisha watendaji wetu kuhusu suala zima la itifaki. Hii itatusaidia katika utendaji wetu wa kazi, kuhakikisha kwamba tunafanya kazi zetu kwa kufuata ustaarabu, staha, adabu na heshima kama ilivyo katika taratibu,” amesema Pallangyo.

Pallangyo amesema mafunzo hayo yameongeza uelewa wa kiutendaji kuhusu itifaki, hasa kwa kuzingatia mazingira ya kazi ambayo yanahitaji watendaji kuwa na uwezo wa kutumia maarifa hayo katika mazingira halisi.

Amesema washiriki wamejifunza namna ya kuwahudumia wananchi na wageni, namna ya kukaa na viongozi, kuwasiliana nao, kuvaa kulingana na mazingira pamoja na kufuata taratibu za kiitifaki katika shughuli mbalimbali.

Habari Picha 21262
Habari Picha 21263

“Tumeambiwa kwamba itifaki ni utaratibu ambao unatakiwa kufuatwa. Tunaamini kwamba tukifuata utaratibu huu katika utendaji wetu wa kazi, utaboresha sana mahusiano yetu na ustaarabu wa kufanya kazi, na hivyo tutaweza kuwahudumia vizuri wananchi ambao tunafanya kazi kwa ajili yao,” amesema Pallangyo.

Afisa TAKUKURU: Mafunzo yametusaidia kutambua makosa ya kiitifaki

Kwa upande wake, Nyasonga Kristopha, Afisa Uchunguzi kutoka TAKUKURU Mkoa wa Arusha, amesema mafunzo hayo yamewasaidia kufahamu taratibu wanazopaswa kuzingatia wanapokuwa katika mazingira ya kikazi, hususan wanapokutana na viongozi wa ngazi mbalimbali.

Amesema kabla ya kupata mafunzo hayo, baadhi ya watendaji walikuwa wanaweza kufanya makosa ya kiitifaki bila kutambua kuwa walikuwa wamekiuka taratibu.

Habari Picha 21257

“Mafunzo haya yametusaidia sisi kama maafisa wa TAKUKURU kujua na kufahamu taratibu mbalimbali ambazo tunatakiwa kuzizingatia tunapokuwa na viongozi, hasa viongozi wetu wa ngazi za juu. Pia yametusaidia namna ya kujiendesha sisi wenyewe kama watumishi katika ofisi zetu,” amesema Kristopha.

Amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa watumishi wa umma kwa kuwa yamewapa uelewa wa vitendo kuhusu namna ya kuzingatia taratibu za kiitifaki katika utekelezaji wa majukumu yao.

Habari Picha 21270

“Kabla ya hapo hatukuwa na mafunzo haya. Kwa hiyo, kwa namna moja au nyingine, tulikuwa tunajikuta tumefanya makosa ya kiitifaki bila hata kujua kwamba tumekosea. Lakini baada ya kupata mafunzo haya, nadhani kwa namna moja au nyingine yametusaidia sana katika masuala haya ya kiitifaki,” amesema Kristopha.

Habari Picha 21264
Habari Picha 21265

Mafunzo yaimarisha utoaji wa huduma za serikali

Mafunzo hayo yamehusisha watendaji kutoka taasisi mbalimbali za serikali na yamelenga kuimarisha uelewa kuhusu heshima, staha, mawasiliano, weledi na uzingatiaji wa taratibu za kiitifaki katika utekelezaji wa majukumu ya umma.

Habari Picha 21266
Habari Picha 21267

Hatua hiyo pia inalenga kuwasaidia watendaji kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia taratibu zinazotakiwa, huku wakidumisha mahusiano mazuri na viongozi, taasisi mbalimbali na wananchi wanaowahudumia.

Habari Picha 21269

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment