HAI, KILIMANJARO:
Serikali ya Kijiji cha Mkombozi, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, imewataka wananchi kuchukua tahadhari mapema kutokana na utabiri wa mvua kubwa zinazohusishwa na hali ya El Niño, huku ikisisitiza umuhimu wa wananchi kufuatilia taarifa rasmi kutoka mamlaka husika.
Hatua hiyo imekuja sambamba na maandalizi ya Serikali ya kijiji hicho kuwa na jengo maalum la dharura litakalotumika kuwahifadhi wananchi watakaoweza kuathirika na maafa yanayoweza kusababishwa na mvua hizo.
Maandalizi hayo yanalenga kuhakikisha kuwa endapo kutatokea mafuriko au maafa mengine na baadhi ya wananchi kukosa maeneo salama ya kukaa, wanapata sehemu ya muda kwa ajili ya usalama na hifadhi.

Wananchi Watakiwa Kuchukua Tahadhari
Hayo yamebainishwa Septemba 16, 2026, katika mkutano wa kawaida wa Kijiji uliofanyika katika viwanja vya kijiji hicho, ambapo wananchi walijadili masuala mbalimbali ya maendeleo pamoja na changamoto zinazowakabili na namna ya kuzitatua.
Miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa ni ujenzi wa shule ya awali na uboreshaji wa barabara, hatua zinazolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma na usafiri kwa wananchi wa kijiji hicho.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkombozi, Julius Malya, amewataka wananchi kuzingatia maelekezo ya tahadhari yanayotolewa na mamlaka husika kuhusu mvua za El Niño.
“Ni kweli Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari kuhusu uwezekano wa mvua za El Niño kuanzia Oktoba hadi Desemba. Wananchi wanahimizwa kuchukua tahadhari kutokana na madhara yanayoweza kujitokeza,” amesema Julius.
Tahadhari Katika Maeneo Hatarishi.
Julius amesema wananchi wanapaswa kufuatilia taarifa na maelekezo rasmi kutoka Serikali na mamlaka husika, huku akiwataka kuepuka maeneo hatarishi, ikiwemo mabondeni, kwenye mikondo ya maji na njia za maji.
Amesema wananchi wanaoishi katika maeneo yenye hatari wanapaswa kuwa tayari kuhama pale itakapoelekezwa na mamlaka husika, ili kuepusha madhara yanayoweza kusababishwa na mafuriko au majanga mengine.


Aidha, amewataka viongozi wa vitongoji na wajumbe wa Serikali ya kijiji kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kukabiliana na athari za mvua kubwa.
Amesisitiza umuhimu wa usafi wa mazingira, hususan kusafisha mifereji na njia za maji ili kuruhusu maji kupita vizuri, pamoja na kupogoa miti iliyo karibu na nyumba ambazo inaweza kusababisha madhara wakati wa mvua na upepo mkali.
Jengo la Dharura Kuwaokoa Wahanga wa Maafa.
Katika hatua nyingine, Serikali ya Kijiji cha Mkombozi imeeleza kuwa imejiandaa kwa kuweka jengo litakalotumika kama eneo la muda la kuwahifadhi wananchi endapo maafa yatatokea.
Jengo hilo linatarajiwa kusaidia wananchi ambao wanaweza kupoteza makazi au kushindwa kurejea katika nyumba zao kutokana na athari za mafuriko au majanga mengine.
Wananchi wamepongeza hatua hiyo, wakisema maandalizi ya mapema ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa jamii pale maafa yanapotokea.
Wananchi Wapongeza Miradi ya Maendeleo
Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo, akiwemo Magret Lymo na Rundyaeli Masawe, wameipongeza Serikali ya Kijiji kwa hatua mbalimbali za kuleta maendeleo katika eneo hilo.
Wamesema ujenzi wa shule ya awali utasaidia kupunguza umbali ambao watoto wadogo hulazimika kutembea ili kupata elimu, huku mpango wa kuboresha barabara kwa kiwango cha moramu ukitarajiwa kurahisisha usafiri ndani ya kijiji na maeneo jirani.


Wananchi hao pia wamepongeza maandalizi ya Serikali ya kijiji ya kuwa na maeneo ya kuwahifadhi wananchi endapo kutatokea maafa na baadhi yao kukosa sehemu salama ya kukaa.
Kwa ujumla, mkutano huo umejadili masuala ya maendeleo na usalama wa wananchi, huku viongozi wa kijiji wakisisitiza umuhimu wa maandalizi ya mapema, ushirikiano wa wananchi na ufuatiliaji wa taarifa rasmi ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa.
Mwisho…
