Na Bahati .SIHA, KILIMANJARO —
Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, umetangaza mpango wa kutembelea wananchi katika kata mbalimbali za wilaya hiyo, nyumba kwa nyumba, kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu hatua za tahadhari dhidi ya mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha katika kipindi kijacho.
Mpango huo umetangazwa na Katibu wa UVCCM Wilaya ya Siha, Sitta Nyakizaza, Septemba 15, 2026, wakati akizungumza katika kikao cha kawaida cha Baraza la UVCCM kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi Kuu ya CCM wilayani humo.

Nyakizaza alisema kikao hicho kilijadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya wilaya, changamoto zinazowakabili wananchi pamoja na namna ya kuzitafutia ufumbuzi. Aidha, wajumbe waliona umuhimu wa UVCCM kushiriki katika kutoa elimu ya tahadhari kwa wananchi kutokana na utabiri wa mvua hizo.
Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanapata taarifa mapema na kuchukua tahadhari zinazofaa ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo.
“Ni kweli, pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo, ikiwamo changamoto na namna ya kuzitatua, tumeona pia tujitoe kwenda kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya mvua hizo zilizotajwa kuwa na madhara,” alisema Nyakizaza.

Kwa mujibu wa Nyakizaza, lengo kuu la mpango huo ni kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kuchukua hatua za tahadhari mapema, huku akisisitiza kuwa usalama wa wananchi ndio kipaumbele.
Hivi karibuni, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa tahadhari kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa mvua za El Niño katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba, na kuwataka wananchi kuchukua hatua za tahadhari kulingana na maelekezo ya mamlaka husika.
UVCCM Yapongeza Uteuzi wa Viongozi.
Katika kikao hicho, UVCCM Wilaya ya Siha pia ilitoa pongezi kwa uongozi wa CCM Taifa kwa uteuzi mbalimbali uliofanyika ndani ya chama.
Umoja huo ulipongeza uteuzi wa Aggrey Mwanri kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara pamoja na Chacha Matiko kwa nafasi ya Katibu wa NEC Taifa, huku ukieleza kuwa uteuzi huo unatarajiwa kuleta nguvu na mwelekeo mpya katika utekelezaji wa majukumu ya chama.
Aidha, UVCCM Siha ilitoa pongezi kwa uteuzi wa Deogratius Ndejembi kuwa Makamu wa Rais, huku ikimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaamini vijana na kuwapa nafasi katika uongozi.
Kwa mujibu wa UVCCM Siha, ushiriki wa vijana katika nafasi za uongozi ni sehemu muhimu ya kuwajengea uzoefu na kuwaandaa kwa majukumu makubwa zaidi ya uongozi.
Katibu CCM Siha: “Chama Kwanza, Mtu Baadaye”
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Siha, Andrea Gwaje, amewataka viongozi na wanachama wa UVCCM kutanguliza maslahi ya chama badala ya watu binafsi.
Gwaje, ambaye pia ni mlezi wa jumuiya hiyo wilayani Siha, aliwataka vijana kuhakikisha kuwa wanabaki na msimamo wa kukitumikia chama na kutokujenga utegemezi mkubwa kwa mtu mmoja mmoja.
“Mimi kama mlezi wa jumuiya hiyo, nawasihi wasiwe karibu sana na mtu kwa kiwango kikubwa. Chama kiwe kitu cha kwanza, mtu anakuja baadaye,” alisema Gwaje.
Alisema msimamo huo utasaidia kuhakikisha UVCCM inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi, kanuni na malengo ya Chama cha Mapinduzi.

Kikao hicho kilihitimishwa kwa msisitizo wa kuendelea kushirikiana na wananchi katika masuala ya maendeleo, huku UVCCM Siha ikijiandaa kutekeleza mpango wake wa kutoa elimu ya tahadhari kuhusu mvua zinazotarajiwa.
Mwisho…
