
Na Mwandishi wa A24tv .
DODOMA:
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemtaka Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, kutumikia nchi kwa utii, uaminifu, uzalendo, utu, busara, hekima na maarifa, huku akitanguliza maslahi ya Taifa.
Rais Samia ametoa maelekezo hayo leo, Agosti 29, 2026, katika hafla ya uapisho wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma.
Amesema nafasi ya Makamu wa Rais ni dhamana aliyopewa na Watanzania, hivyo Mhe. Ndejembi anatakiwa kuitumia kwa kuwatumikia wananchi wote bila kujali tofauti zao, sambamba na kuhakikisha majukumu anayokabidhiwa yanatekelezwa kwa maslahi mapana ya Taifa.
Rais Samia pia amesisitiza umuhimu wa bidii, nidhamu, weledi na utayari wa kujifunza katika kutekeleza majukumu hayo, akibainisha kuwa hakuna shule inayofundisha nafasi ya Makamu wa Rais.
Amesema kujifunza katika nafasi hiyo kunahusisha kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali, pamoja na kujifunza kutokana na uzoefu wa viongozi wengine anaofanya nao kazi.
Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa cheo cha Makamu wa Rais si ufalme bali ni dhamana ya kuwatumikia wananchi. Kwa msingi huo, amemtaka Mhe. Ndejembi kulitambua hilo na kuendelea kuitumikia Tanzania kwa uaminifu, uwajibikaji na uzalendo.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amesema utekelezaji wa majukumu ya Serikali unahitaji umoja, mshikamano, ushirikiano, utulivu na uongozi bora ili kufikia matamanio na matarajio ya Watanzania.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Makamu wa Rais na viongozi wengine ndani ya Serikali ni muhimu katika kuhakikisha majukumu yanatekelezwa kwa ufanisi na malengo ya maendeleo yanafikiwa kwa kuzingatia maslahi na usawa wa wananchi wote.
Rais Samia amemtaka Mhe. Ndejembi kutumia nafasi hiyo kwa busara na hekima, akizingatia kuwa dhamana aliyopewa ni ya wananchi na kwamba kila hatua anayochukua inapaswa kuelekezwa katika kulinda na kuendeleza maslahi ya Taifa.

