HONGERA TRA KWA KUTIMIZA MIAKA 30 YA KUIJENGA NCHI YETU.

Geofrey Steven
1 Min Read

Dodoma, Agosti 7, 2026

Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kutimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, akisema mafanikio yaliyopatikana kupitia ukusanyaji wa mapato yamechangia maendeleo ya nchi na uboreshaji wa miundombinu.

Habari Picha 19830
Habari Picha 19829

Pongezi hizo amezitoa leo, Agosti 7, 2026, jijini Dodoma alipotembelea banda la TRA lililopo ndani ya Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samuel John Malecela, Dodoma, ambapo pia amesifu jitihada za TRA katika kuongeza ukusanyaji wa mapato nchini.

Mhe. Chongolo amesema TRA ni kiungo muhimu katika uletaji wa maendeleo nchini, kwa kuwa mapato yanayokusanywa kupitia kodi yameiwezesha Serikali kuboresha miundombinu na kuchochea ukuaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo sekta ya kilimo.

“TRA ndio injini ya uletaji wa maendeleo kwa sababu kupitia makusanyo ya kodi wanayofanya, yamepelekea ukuaji mkubwa wa maendeleo nchini kwetu,” amesema Mhe. Chongolo.

Habari Picha 19831

Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayoendelea jijini Dodoma yametoa fursa kwa wakulima, wafanyabiashara na walipakodi kupata elimu na huduma mbalimbali kutoka TRA, pamoja na kujifunza kuhusu umuhimu wa ulipaji kodi katika kuchochea maendeleo ya taifa.

Maonesho hayo yanatarajiwa kufikia kilele chake kesho, Agosti 8, 2026.

 

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment