TIDI YATOA MATIBABU BURE KWA WANANCHI WA SIHA KUSHEREHEKEA MIAKA 100 YA HUDUMA.

Geofrey Steven
6 Min Read

Na Mwandishi wa A24tv. SIHA:

Katika kuadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake, Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza Tanzania (TIDI) imeandaa kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu bure kwa wananchi wa Wilaya ya Siha na maeneo jirani, ikiwa ni sehemu ya kurudisha fadhila kwa jamii iliyokuwa ikiunga mkono taasisi hiyo kwa miaka mingi.

Kambi hiyo ya siku nne imeanza Novemba 5, 2026, katika viwanja vya Kibong’oto na inatarajiwa kumhudumia idadi kubwa ya wananchi kwa kuwapatia huduma mbalimbali za afya bila malipo hadi Novemba 8, 2026.

Habari Picha 22208

Huduma zinazotolewa katika kambi hiyo ni pamoja na uchunguzi wa afya unaofanywa na madaktari bingwa, ushauri wa kitaalamu na matibabu ya magonjwa mbalimbali. Pia wananchi wanapata fursa ya kupima shinikizo la damu, kisukari, macho, meno, pamoja na magonjwa ya kawaida. Aidha, kuna huduma za ushauri wa lishe bora kwa wajawazito na watoto.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo, Mkurugenzi wa TIDI, Dkt. Leonard Subi, amesema kufikisha miaka 100 kwa taasisi hiyo ni mafanikio makubwa yaliyotokana na neema ya Mungu pamoja na ushirikiano na msaada wa wananchi.

 

Habari Picha 22205
Habari Picha 22206

Amesema taasisi hiyo imeona ni muhimu kusherehekea hatua hiyo kwa kuwagusa wananchi moja kwa moja kupitia huduma za afya bila malipo.

“Tumefikia miaka 100 kwa neema ya Mungu na msaada wa wananchi. Hatuwezi kusherehekea peke yetu wakati wananchi wanaumwa. Ndiyo maana tumekuja kutoa huduma hii bure kama shukrani na kurudisha kwa jamii,” amesema Dkt. Subi.

Ameongeza kuwa lengo la kambi hiyo ni kuwasaidia wananchi kufahamu hali za afya zao kupitia uchunguzi wa kitaalamu ili waweze kuchukua hatua mapema, kupata matibabu na kuendelea kuwa na afya bora kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na uchumi wa Taifa.

Dkt. Subi ameeleza kuwa wagonjwa watakaobainika kuwa na changamoto za kiafya zinazohitaji uangalizi zaidi wataunganishwa na vituo vya kutolea huduma za afya vinavyoweza kuwapatia matibabu na ufuatiliaji unaostahili.

Amesema TIDI imekuwa na utaratibu wa kuendesha kambi za aina hiyo katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo Mkoa wa Arusha, mikoa ya Kanda ya Ziwa na Tanga. Hivyo, katika maadhimisho ya miaka 100, taasisi imeona umuhimu wa kuhakikisha wananchi wanashiriki na kunufaika moja kwa moja na mafanikio ya taasisi hiyo.

Kambi hiyo imewashirikisha madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mawenzi, Hospitali ya Wilaya ya Siha pamoja na wataalamu kutoka TIDI.

Kwa upande wao, wananchi waliojitokeza kupata huduma hizo wameishukuru TIDI kwa kuwafikishia huduma za afya karibu na maeneo yao, hasa kutokana na changamoto za gharama za matibabu ambazo zimekuwa zikikwamisha baadhi yao kupata huduma hospitalini.

Habari Picha 22207

Mmoja wa wananchi hao, Leonard Kileo, mkazi wa Kashashi wilayani Siha, amesema amepata fursa ya kupima shinikizo la damu, macho na kufanyiwa uchunguzi wa miguu yake ambayo imekuwa ikimsababishia changamoto ya kutembea vizuri.

Amesema awali alikuwa akishindwa kwenda hospitalini kutokana na gharama za matibabu, hivyo ametoa shukrani kwa taasisi hiyo kwa kuwajali wananchi, hususan wazee.

“Nawashukuru sana kwa kutukumbuka, hasa sisi wazee. Nimepata huduma mbalimbali bure kabisa, jambo ambalo limenisaidia kwa sababu gharama za kwenda hospitalini zimekuwa changamoto kwangu,” amesema Kileo.

Kwa upande wa Serikali, Katibu Tawala wa Wilaya ya Siha, Jane Chalamila, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Christopher Timbuka, ameipongeza TIDI kwa hatua ya kuandaa kambi hiyo na kutoa huduma za afya bila malipo kwa wananchi.

Amesema Hospitali ya Kibong’oto imekuwa na historia kubwa katika sekta ya afya nchini, hususan katika mapambano dhidi ya kifua kikuu, ikiwemo kifua kikuu sugu, na kwamba kupanuka kwa wigo wa huduma zake hadi kuwa Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza Tanzania ni hatua muhimu katika kuimarisha huduma za afya nchini.

Habari Picha 22204

Ameeleza kuwa kuanzishwa kwa taasisi hiyo kumeongeza uwezo wa Taifa katika utoaji wa huduma bingwa, uchunguzi, utafiti, mafunzo na mwitikio wa kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza.

Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake na juhudi za kuimarisha taasisi hiyo, ambayo ni muhimu katika kulinda afya na usalama wa wananchi.

Chalamila amesisitiza kuwa kambi hiyo ni jambo la kizalendo linaloonesha dhamira ya taasisi katika kuirudishia jamii kile ilichonufaika nacho kwa miaka mingi, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma zinazotolewa.

Amefafanua kuwa huduma hizo zinajumuisha uchunguzi wa magonjwa ya mapafu, magonjwa ya kuambukiza, kisukari, shinikizo la damu, macho, masikio, meno na mifupa, pamoja na huduma nyingine za uchunguzi na ushauri wa kitaalamu.

Habari Picha 22209

Katika kuhitimisha maadhimisho hayo ya miaka 100, TIDI pia imeandaa mashindano ya mbio za Marathon yatakayofanyika Novemba 8, 2026, katika viwanja vya Kibong’oto, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa mazoezi na afya bora.

Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment