WAFANYABIASHARA WATAHADHARISHA SHERIA ZISIPOTEZE FURSA ZA UWEKEZAJI.

Geofrey Steven
4 Min Read

Na mwandishi wetu A24 Tv

Wafanyabiashara nchini wametaka Serikali na taasisi zinazohusika na sekta ya biashara kuhakikisha sheria na kanuni zinazosimamia shughuli za kibiashara zinafahamishwa kwa kina kwa wafanyabiashara kabla ya kuchukua hatua za utekelezaji, wakionya kuwa ukosefu wa elimu unaweza kusababisha mkanganyiko na kuathiri mazingira ya biashara nchini.

Wito huo umetolewa Novemba 4,2026 Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara na Huduma Tanzania (UWAHUTA), Martin Mbwana wakati akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake amesisitiza umuhimu wa Serikali, vyama vya wafanyabiashara na taasisi nyingine zinazohusika na sekta hiyo kushirikiana katika kutoa elimu kwa wafanyabiashara wazawa na wageni kuhusu matakwa ya sheria.

“Kuhusu wageni.

Habari Picha 22112

Sheria imeshatungwa kinachotakiwa ni uelewa wa pamoja kwa kushirikisha vyama vyote na tqasisi zote za kibiashara ndipo sheria ifuate mkondo wake sababu wageni hawa tumewapangisha,tunanunua katika maduka yao ,tunaishi nao ni majirani zetu kuanza operation ya kutumia mabavu haina afya katika biashara na mahusiano yetu”

Mbwana amesema badala ya kukimbilia kuchukua hatua zinazoweza kusababisha kufungwa kwa maduka au kuibua mkanganyiko kuhusu nani anaruhusiwa kufanya biashara fulani, ni muhimu kwanza kuhakikisha wahusika wanaelewa sheria, malengo yake na namna inavyopaswa kutekelezwa.

Amesema wafanyabiashara wa kigeni hawapaswi kuchukuliwa kama kundi moja, kwa kuwa mazingira yao ya uwekezaji na shughuli wanazofanya yanatofautiana, akieleza kuwa baadhi wana mitaji mikubwa huku wengine wakifanya shughuli zao kwa kushirikiana na wazawa katika majengo na maghala yanayomilikiwa na Watanzania.

Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya wazawa na wageni ni muhimu katika kukuza biashara na kwamba taasisi kama Chama cha Taifa cha Biashara Tanzania (TNCC) pamoja na wadau wengine zinapaswa kuwa sehemu ya juhudi za kuelimisha na kujenga uelewa wa pamoja.

Katika hatua nyingine, Mbwana ameeleza kuwa mabadiliko ya soko la saruji yanaonesha umuhimu wa kuimarisha uzalishaji wa ndani, akibainisha kuwa bei ya bidhaa hiyo iliwahi kupanda hadi Sh 15,000, Sh 16,000 na Sh 20,000 na 21,000 na haijashuka mpaka sasa kutokana na kusimama kwa uzalishaji katika kiwanda cha Dangote na kuongezeka kwa mahitaji.

Amesema kurejea kwa uzalishaji katika kiwanda hicho kunatarajiwa kusaidia kurejesha utulivu wa bei, hasa ikizingatiwa mahitaji makubwa ya saruji yanayotokana na miradi mbalimbali ya maendeleo na ujenzi nchini.

Kuhusu mwenendo wa biashara kwa ujumla, Mbwana amesema soko limeonesha utulivu, huku thamani ya dola ikiwa imetulia na shughuli za usafirishaji wa mizigo kupitia meli zikiendelea bila changamoto kubwa, hali inayoweza kusaidia wafanyabiashara kupanga shughuli zao kwa uhakika zaidi.

Hata hivyo, amesema mapinduzi ya teknolojia yamebadilisha kwa kiasi kikubwa namna biashara zinavyofanyika duniani, akieleza kuwa mfanyabiashara anaweza kuwa nchini Tanzania, kuagiza bidhaa kutoka nje, kufanya malipo kupitia benki na taasisi za kifedha za kimataifa na kupokea mzigo moja kwa moja dukani kwake.

Amesema mabadiliko hayo yanahitaji Serikali na sekta binafsi kushirikiana kuweka mazingira na miundombinu rafiki inayowezesha wafanyabiashara kutumia fursa za biashara mtandao, huku wakizingatia mabadiliko ya mifumo ya biashara ya kimataifa.

Ameeleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu ili wafanyabiashara wazawa na wageni waweze kushindana katika soko la kisasa, kukuza biashara na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.

Mbwana amehimiza wadau wa biashara kutambua kuwa uelewa wa sheria, matumizi ya teknolojia na ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni mambo yanayohitaji kwenda sambamba ili kujenga mazingira endelevu ya biashara nchini.

Share This Article
Leave a Comment