MISS BANTU APATOSHI TANZANIA YAPAMBA MOTO ARUSHA: USAJILI WAANZA KWA KISHINDO NOVEMBA 10, MSHINDI KUTWAA GARI ZITO, WADHAMINI WAFUNGULIWA MILANGO.

Geofrey Steven
4 Min Read

ARUSHA:

Mashindano mapya ya urembo wa asili wa mwanamke wa Kiafrika, Miss Bantu Tanzania, yanatarajiwa kupamba anga la burudani nchini baada ya kutangazwa rasmi kwa kuanza kwa usajili wa washiriki Novemba 10, 2026, jijini Arusha.

Habari Picha 22034

Shindano hilo linaloingia kwa mara ya kwanza katika tasnia ya urembo nchini linakuja na dhana tofauti na mashindano mengi yanayofahamika, likilenga kuutukuza urembo wa asili wa mwanamke wa Kiafrika bila kubagua maumbo ya mwili wala urefu.

Msisimko zaidi umeongezeka baada ya waandaaji kueleza kuwa mshindi wa shindano hilo anatarajiwa kuondoka na zawadi ya gari, huku wadhamini na kampuni mbalimbali wakikaribishwa kuungana na waandaaji kufanikisha tukio hilo kubwa la burudani na uwezeshaji wa wanawake.

Habari Picha 22033

Usajili wa washiriki utafanyika katika viunga vya Makumbusho ya Azimio la Arusha, huku shindano hilo likiwalenga wanawake wenye umri wa miaka 18 hadi 45.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha Oktoba 30, 2026, mshirika mwenza wa Miss Bantu Tanzania, Jackline Kesi, alisema shindano hilo limeanzishwa kwa lengo la kwenda zaidi ya kutafuta mshindi wa taji la urembo, bali kumtambua mwanamke wa Kiafrika, kuthamini utamaduni wake na kumfungulia milango ya fursa za kiuchumi.

Alisema Miss Bantu Tanzania ni jukwaa litakalowapa wanawake nafasi ya kuonyesha vipaji, uwezo, ubunifu na mchango wao katika jamii, huku likiwawezesha kujitegemea kupitia fursa zitakazopatikana ndani na nje ya mashindano hayo.

Kwa upande wake, mwalimu wa mamiss na wanamitindo, Lisa Steven, maarufu kama Lislamod, alisema Miss Bantu inalenga kuvunja mitazamo iliyojengeka katika jamii kuhusu vigezo vya urembo, hasa dhana kwamba mwanamke mzuri lazima awe na urefu au umbo fulani.

Alisema shindano hilo linatoa nafasi kwa wanawake wa maumbo mbalimbali kushiriki na kusherehekea uzuri wao wa asili, huku afya, uwezo na vipaji vikitazamwa kuwa sehemu muhimu ya thamani ya mshiriki.

Lisa alibainisha kuwa washiriki watapata fursa za mafunzo, kushirikishwa na kampuni na taasisi mbalimbali pamoja na kupata nafasi za kuwa mabalozi wa bidhaa na huduma (brand ambassadors).

Aliongeza kuwa ushirikiano na wadhamini utakuwa na mchango mkubwa katika kufungua fursa za ajira na kipato kwa washiriki, huku ukiwasaidia kujenga uwezo wa kujitegemea hata baada ya kumalizika kwa mashindano.

Katika hatua nyingine, Afisa Utamaduni wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Benson Maneno, aliyemwakilisha Mkuu wa Kitengo cha Sanaa na Utamaduni, alisema halmashauri imekabidhi kibali cha Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa taasisi ya Hibri Institute of Technology, kinachoiruhusu kuendesha mashindano hayo katika wigo wa kitaifa.

Maneno aliwapongeza waandaaji kwa hatua hiyo na kueleza kuwa halmashauri inatambua umuhimu wa wadau wa sanaa na utamaduni katika kukuza vipaji, ubunifu na kuitangaza jamii kupitia shughuli za kisanaa.

Habari Picha 22035
Habari Picha 22036

Aidha, aliwataka waandaaji kutumia jukwaa hilo kushiriki katika kampeni za kuhamasisha michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), akieleza kuwa washiriki wanaweza kuwa sehemu ya kuitangaza Tanzania na kuhamasisha wananchi kuelekea mashindano hayo makubwa ya soka.

Alisema matarajio ya halmashauri ni kuona washiriki wa Miss Bantu wakishiriki shughuli za hamasa kuelekea AFCON na kuwepo katika mechi ya ufunguzi itakayofanyika Uwanja wa Samia.

Kwa ujumla, Miss Bantu Tanzania inaonekana kuja na sura mpya katika tasnia ya mashindano ya urembo nchini, ikichanganya burudani, utamaduni, ujasiriamali na uwezeshaji wa wanawake.

Huku usajili ukitarajiwa kuanza Novemba 10, macho ya wapenzi wa burudani yanaelekezwa Arusha kuona ni nani atakayejitokeza kuwania taji hilo na hatimaye kuandika historia kama mshindi wa kwanza wa Miss Bantu Tanzania.

WITO KWA WADHAMINI:

Kampuni, taasisi na wadau wa biashara wanakaribishwa kuungana na waandaaji wa Miss Bantu Tanzania kwa kudhamini shindano hilo na kuwa sehemu ya jukwaa linalolenga kukuza vipaji, kuenzi utamaduni wa Kiafrika na kufungua fursa za kiuchumi kwa wanawake wa Kitanzania.

 

Mwisho ..

Share This Article
Leave a Comment