Na Richard Mrusha A24TV
Bokgoni Matla yasisitiza matumizi ya takwimu kufanya maamuzi ya kibiashara, yaeleza kuwa kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani ndio ufunguo wa kutatua changamoto za Kiafrika
Kampuni za madini barani Afrika zimetakiwa kuwekeza katika matumizi sahihi ya data na kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani ili kuboresha maamuzi, kuongeza ufanisi wa uzalishaji na kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje.

Wito huo umetolewa Oktoba 30,2026 kwenye maonesho ya 10 ya Madini Afrika na Melvin Ekandjo, Mkurugenzi Mkuu na mshirika mkuu wa kampuni ya Bokgoni Matla ya Pretoria, Afrika Kusini, inayolenga kusaidia mashirika katika sekta ya madini na maeneo mengine ya biashara kutumia data kutambua changamoto na kupata suluhisho zinazotokana na ushahidi.
Amesema licha ya data kuwa nyenzo muhimu katika maendeleo ya biashara za kisasa, baadhi ya kampuni bado hazitumii kikamilifu taarifa walizonazo, hali inayoweza kuzifanya zikose fursa za kuboresha utendaji na kufanya maamuzi yenye tija.
Akanjo ameeleza kuwa data haipaswi kuchukuliwa kama mkusanyiko wa takwimu pekee, bali ni nyenzo inayosaidia taasisi kuelewa mazingira yake, kutathmini utendaji na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho.

Kwa mujibu wake, kampuni zinazoweza kuchambua na kutumia taarifa zake kwa usahihi zina nafasi kubwa ya kuelewa changamoto zinazozikabili na kutafuta njia zinazofaa za kuzitatua.
Akizungumzia namna Afrika inavyoweza kukabiliana na changamoto zake, Ekandjo amesisitiza umuhimu wa kujenga uwezo wa ndani badala ya kutegemea wataalamu wa nje kila mara kunapojitokeza tatizo.
Amesema maendeleo endelevu yanahitaji watu wenye maarifa na ujuzi wa kutambua matatizo katika mazingira yao, kuchambua taarifa zilizopo na kubuni suluhisho zinazoweza kutekelezeka.
Ameeleza kuwa data ni miongoni mwa nyenzo muhimu katika kufanikisha azma hiyo, lakini haiwezi kuleta matokeo yaliyokusudiwa bila kuwekeza kwa watu wanaopaswa kuichambua na kuitumia.
Kwa msingi huo, amesisitiza mafunzo na ukufunzi kazini kuwa sehemu muhimu ya kujenga uwezo wa wafanyakazi ili waweze kutumia taarifa zilizopo katika kufanya maamuzi na kuboresha utendaji wa mashirika yao.
Katika kusaidia mashirika kufikia malengo hayo, Bokgoni Matla hutoa mafunzo na ukufunzi unaolenga kuwajengea watu uwezo wa kutumia data katika kutatua changamoto halisi za kiutendaji.
Ekandjo amesema kampuni hiyo pia hutumia uigaji wa mazingira ya kazi ili kuwasaidia washiriki kuelewa namna taarifa zinavyoweza kutumika katika mazingira yanayofanana na shughuli halisi za mashirika yao.
Amesema njia hiyo husaidia washiriki kupata uelewa wa vitendo kuhusu namna ya kuchambua changamoto na kutumia data kutafuta suluhisho zinazoweza kuboresha utendaji.
Kwa mujibu wake, lengo si kuwapa watu takwimu pekee, bali kuwawezesha kuzitumia katika kazi zao za kila siku na kuzifanya kuwa sehemu ya utamaduni wa kufanya maamuzi ndani ya taasisi.
Ekandjo amesema mwitikio walioupata kutoka kwa washiriki na wadau umeonesha kuwa matumizi ya data yana umuhimu katika maeneo mengi ya utendaji wa taasisi, yakiwemo rasilimali watu, uendeshaji na mauzo.
Amesema mawasiliano na maswali kutoka kwa wadau wa sekta mbalimbali yamewapa nafasi ya kueleza namna data inavyoweza kutumika kutatua changamoto zinazojitokeza katika mazingira tofauti ya kazi.
Kwa sekta ya madini, matumizi hayo yanaweza kusaidia mashirika kuchambua taarifa za uzalishaji, kufuatilia utendaji na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho, kutegemea aina na ubora wa data zinazokusanywa.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya mabadiliko hayo yanategemea uwezo wa watu kutafsiri taarifa na kuzigeuza kuwa maamuzi yenye tija, na kuwa watu wanapaswa kuendelea kuwa kiini cha mabadiliko licha ya umuhimu wa teknolojia.
