Yalenga ubia kati ya wazawa na wawekezaji wa nje; eneo la Buzwagi la ekari zaidi ya 127 kutumika kuvutia uwekezaji na kuimarisha maudhui ya ndani
Chama cha Watoa Huduma na Wasambazaji wa Bidhaa Migodini (TAMISA) kimeweka mkazo katika kuanzisha viwanda nchini kupitia ubia kati ya kampuni za Kitanzania na wawekezaji wa nje, kikilenga kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinazotumika migodini na kupanua fursa za kiuchumi kwa wazawa.
Hayo yamebainishwa Leo Oktoba 28,2026 Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya 10 ya Madini Afrika na Afisa Mtendaji Mkuu wa TAMISA, Jaffet Mussa, alisema mpango huo unalenga kutumia fursa zinazopatikana katika sekta ya madini kuvutia mitaji, teknolojia na utaalamu kutoka nje, huku ukijenga uwezo wa kampuni za ndani kushiriki zaidi katika mnyororo wa thamani wa madini.

Alisema TAMISA, ambayo ni miongoni mwa waandaaji wa maonesho ya Mining Expo Africa yanayofanyika kwa mara ya 10, inatumia jukwaa hilo kuwaunganisha wazawa na kampuni za kimataifa ili kujenga ushirikiano wa kibiashara na kuwezesha upatikanaji wa teknolojia na mitambo ya kisasa.
Kwa mujibu wa Mussa, ushirikiano huo unaweza kusaidia kampuni za Kitanzania kuanzisha uzalishaji wa bidhaa zinazohitajika migodini badala ya kutegemea zaidi bidhaa kutoka nje, hatua inayoweza kuongeza fursa za biashara kwa wazawa na kuchochea maendeleo ya viwanda nchini.
Katika kuimarisha azma hiyo, TAMISA ina eneo maalumu la kiuchumi (Special Economic Zone — SEZ) lililopo Buzwagi, lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 127, ambalo limekusudiwa kupokea wawekezaji wa ndani na nje kwa ajili ya kuanzisha viwanda.

Mussa alisema eneo hilo linatoa fursa kwa wawekezaji wa kigeni kushirikiana na kampuni za Kitanzania kuanzisha uzalishaji wa bidhaa na huduma zinazohitajika katika shughuli za uchimbaji madini.
Alieleza kuwa ushirikiano huo unaweza kuwa njia ya kuhamisha teknolojia na maarifa ya uzalishaji kwenda kwa wazawa, huku ukipanua uwezo wa kampuni za ndani kuhudumia migodi kwa ufanisi zaidi.
Hatua hiyo ina umuhimu katika kuongeza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za kiuchumi zinazozunguka sekta ya madini, ikiwamo utengenezaji wa vifaa, usambazaji wa bidhaa na utoaji wa huduma mbalimbali kwa kampuni za uchimbaji.
Mussa alisema utekelezaji wa sheria, kanuni na sera za maudhui ya ndani (Local Content) una nafasi muhimu katika kuhakikisha kuwa shughuli za madini zinawanufaisha Watanzania kupitia ushiriki wa kampuni za ndani katika kutoa bidhaa na huduma migodini.
Alibainisha kuwa Serikali na Wizara ya Madini zimeweka mifumo ya kuimarisha ushiriki wa wazawa, huku lengo likiwa ni kufikia uwiano wa ndani wa angalau asilimia 90.
Alisema kufikiwa kwa malengo hayo kunahitaji ushirikiano kati ya Serikali, wawekezaji wa kimataifa na kampuni za Kitanzania ili kujenga uwezo wa wazawa katika teknolojia, mitaji na uzalishaji wa bidhaa zinazokidhi mahitaji ya migodi.
Kwa mtazamo huo, maonesho ya 10 ya Madini Afrika yanatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kuwaunganisha wadau hao, kutafuta washirika wa biashara na kuibua fursa za uwekezaji zinazoweza kuimarisha sekta ya huduma na ugavi wa bidhaa migodini.
Ingawa sekta ya madini inahitaji mitambo, teknolojia na bidhaa mbalimbali, ushirikiano kati ya kampuni za ndani na za nje unaweza kusaidia kupunguza utegemezi wa uagizaji wa baadhi ya bidhaa kwa kuwezesha uzalishaji nchini.

Aidha, kuanzishwa kwa viwanda kunatoa fursa za kupanua shughuli za biashara kwa wazawa na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine zinazohusiana na madini.
Hata hivyo, mafanikio ya mpango huo yatategemea uwezo wa kuvutia wawekezaji, upatikanaji wa teknolojia, mitaji na ujuzi, pamoja na utekelezaji madhubuti wa mifumo inayowezesha kampuni za Kitanzania kushindana katika soko la bidhaa na huduma za migodini.
Mwisho..
