Na Geofrey Stephen ARUSHA, OKTOBA 27, 2026
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dkt. Richard Mayungi, amesema ukaguzi wa mazingira unapaswa kwenda zaidi ya kuchunguza matumizi ya fedha za umma na kulenga kuhakikisha rasilimali za asili zinalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Amesema Afrika ina utajiri mkubwa wa rasilimali za asili, ikiwamo misitu, madini, wanyamapori na vyanzo vya maji, hivyo udhaifu katika usimamizi wake unaweza kuathiri uchumi, afya za wananchi na ustawi wa mamilioni ya watu barani Afrika na duniani kwa ujumla.



Dkt. Mayungi aliyasema hayo jijini Arusha wakati akifungua, kwa niaba ya Naibu Waziri, Mkutano Mkuu wa 12 wa Mwaka 2026 wa Kikundi Kazi cha Ukaguzi wa Mazingira cha Shirika la Taasisi za Juu za Ukaguzi Barani Afrika (AFROSAI-WGE), unaowakutanisha washiriki kutoka nchi 32.
Akizungumza katika mkutano huo, alisema ukaguzi wa mazingira una jukumu muhimu katika kuhakikisha sera na sheria za uhifadhi zinatekelezwa ipasavyo, fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya mazingira zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, na serikali zinawajibika kwa matokeo ya hatua zinazochukua.
“Kwa kutafakari umuhimu wa kazi hii, nimejiuliza swali, tunakagua nini kama Afrika na kwa nini kazi hiyo ni muhimu? Jibu langu ni kwamba mnakagua mustakabali wa dunia. Hii si ukaguzi wa mazingira ya Afrika pekee, bali ni ukaguzi wa rasilimali zinazochangia maisha na uchumi wa dunia,” alisema Dkt. Mayungi.
AFRIKA INA WAJIBU MKUBWA KATIKA UHIFADHI WA RASILIMALI.
Dkt. Mayungi alisema umuhimu wa ukaguzi wa mazingira unatokana na nafasi ya Afrika katika uhifadhi wa mifumo ya ikolojia duniani, uzalishaji wa malighafi zinazotumika katika teknolojia za kisasa na usimamizi wa rasilimali za maji zinazotegemewa na nchi nyingi.
Alitaja Bonde la Kongo kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya misitu duniani, huku vyanzo vikubwa vya maji, vikiwamo Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa, vikihitaji usimamizi endelevu ili kulinda upatikanaji wa maji na kupunguza athari za uchafuzi.
Alisisitiza kuwa rasilimali hizo haziwezi kulindwa kwa ufanisi bila mifumo imara ya uwajibikaji, ukaguzi unaotegemea ushahidi na ushirikiano wa nchi zinazotegemeana katika matumizi ya rasilimali zinazovuka mipaka ya kitaifa.
TANZANIA KUIMARISHA UHIFADHI KUPITIA DIRA YA MAENDELEO 2050.
Akizungumzia hatua za Tanzania, Dkt. Mayungi alisema uhifadhi wa mazingira ni sehemu muhimu ya mkakati wa maendeleo ya taifa, kama unavyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia nguzo ya uadilifu wa mazingira na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Alisema nguzo hiyo inalenga kulinda bioanuwai, kusimamia matumizi endelevu ya maji na maeneo oevu, kudhibiti uchafuzi wa mazingira, kuimarisha matumizi bora ya ardhi na kuongeza uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aliongeza kuwa serikali inaendelea kuimarisha mipango ya matumizi ya ardhi, upangaji wa miji unaozingatia mazingira, usimamizi wa taka, uchumi wa mzunguko na matumizi ya nishati safi ili kuoanisha uhifadhi wa mazingira na ukuaji wa uchumi.
Hata hivyo, alisema utekelezaji wa mipango hiyo unahitaji ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha fedha na rasilimali zinazotengwa zinatumika kwa ufanisi na kuleta matokeo yanayopimika kwa wananchi.
KICHERE ATOA WITO WA USHIRIKIANO KATIKA USIMAMIZI WA RASILIMALI ZA MAJI.
Kwa upande wake, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, ambaye ni Mwenyekiti wa AFROSAI, alisema nchi za Afrika zinapaswa kuimarisha ushirikiano katika usimamizi wa rasilimali za maji, kwa kuwa athari za maamuzi yanayofanywa katika nchi moja zinaweza kujitokeza katika nchi nyingine.
Kichere, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kikundi Kazi cha Ukaguzi wa Mazingira cha AFROSAI, alisema taasisi za ukaguzi zinapaswa kubadilishana taarifa na uzoefu ili kubaini changamoto za kimazingira zinazovuka mipaka ya kitaifa na kupendekeza hatua za pamoja za kukabiliana nazo.

Akitolea mfano wa Ziwa Victoria na mfumo wa Mto Nile, alisema rasilimali za maji zinazounganisha nchi mbalimbali zinahitaji usimamizi unaozingatia maslahi ya wananchi wote wanaozitegemea.
Alisisitiza kuwa mipaka ya kisiasa haiwezi kuzuia athari za kimazingira zinazotokana na matumizi ya rasilimali zinazoshirikishwa na nchi mbalimbali.
UKAGUZI UNAPASWA KUZAA MATOKEO, SI RIPOTI PEKEE.
Kichere alisema taasisi za ukaguzi zina wajibu wa kuchunguza iwapo ahadi za mazingira zimejumuishwa katika mipango na bajeti za serikali, fedha za umma zinatumika ipasavyo na miradi inatekelezwa kwa kufikia malengo yaliyowekwa.


Alisema ripoti za ukaguzi zinapaswa kusaidia serikali kubaini mapungufu na kuchukua hatua za kurekebisha kasoro zilizobainika. Aliongeza kuwa matumizi ya teknolojia za kidijitali na mafunzo ya kitaalamu ni muhimu katika kuongeza uwezo wa wakaguzi kutathmini taarifa za uendelevu na kubaini changamoto za usimamizi wa mazingira.
Alisisitiza kuwa mafanikio ya ukaguzi wa mazingira hayapaswi kupimwa kwa idadi ya ripoti zinazotolewa pekee, bali pia kwa hatua zinazochukuliwa kulinda vyanzo vya maji, kudhibiti uchafuzi na kuhakikisha fedha za umma zinaleta manufaa yaliyokusudiwa.
Aidha, aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za ukaguzi, serikali na mabunge, huku wakizingatia umuhimu wa kulinda uhuru wa taasisi za ukaguzi katika kutekeleza majukumu yao.
MKUTANO KUJADILI UCHUMI WA KIJANI NA USALAMA WA MAJI.
Mkutano huo unaofanyika jijini Arusha unajadili namna ukaguzi wa mazingira unavyoweza kuchangia kukuza uchumi wa kijani, kuimarisha usalama wa maji na kudhibiti uchafuzi wa mazingira.



Pia, unalenga kuimarisha uwajibikaji na usimamizi endelevu wa rasilimali za Afrika ili kuchangia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya muda mrefu, ikiwamo azma ya kufikia uchumi wa shilingi trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Washiriki wanatarajiwa kubadilishana uzoefu na kujadili mbinu za kuimarisha ukaguzi wa mazingira ili kuhakikisha rasilimali za asili zinalindwa, fedha za umma zinatumika kwa tija na hatua za uhifadhi zinatoa matokeo yanayowanufaisha wananchi na dunia kwa ujumla.
MWISHO.
