Na Geofrey Stephen Arusha .
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, amesema kuwa hadi sasa washiriki zaidi ya 2,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani wamejisajili kuhudhuria Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), utakaofanyika jijini Arusha.
Mheshimiwa Zungu ameyasema hayo Oktoba 2, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), ambacho kitakuwa mwenyeji wa mkutano huo.
Amesema kuwa hadi sasa nchi 149 zimethibitisha kushiriki mkutano huo, huku nchi nyingine zikiendelea kuwasilisha taarifa za ushiriki wao. Kwa upande wa Tanzania, jumla ya washiriki 147 tayari wamejisajili.

Spika Zungu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa kibali cha kufanyika kwa mkutano huo nchini Tanzania, akieleza kuwa tukio hilo ni fursa muhimu ya kuitangaza nchi kimataifa.
“Natoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa kibali cha Mkutano wa IPU kufanyika Tanzania,” amesema.
Aidha, amewataka wakazi wa Arusha kutumia uzoefu wao wa kupokea wageni na ukarimu wao kuhakikisha washiriki wa mkutano huo wanapata mapokezi mazuri na kujionea utamaduni wa Watanzania.


“Nafahamu watu wa Arusha ni wakarimu na wana uzoefu wa kupokea wageni. Kwa kuwa ninyi ndiyo mnaowakilisha mkoa huu, tunataka wageni wajionee ukarimu wa Watanzania,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa mkutano huo unatoa fursa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wa Arusha na maeneo mengine nchini kutangaza bidhaa na huduma zao, pamoja na kunufaika na fursa zitakazojitokeza katika sekta ya utalii na biashara.
“Tuitumie fursa hii kukuza na kuonyesha biashara zetu. Changamkieni fursa mbalimbali, ikiwemo utalii, ili kuhakikisha uchumi wa Arusha unakua,” amesema.
AIPONGEZA MEDIA KWA KUTANGAZA MKUTANO
Katika hatua nyingine, Spika Zungu amewashukuru waandishi wa habari kwa kuendelea kutangaza na kuhabarisha umma kuhusu maandalizi ya mkutano huo tangu yalipoanza, akibainisha kuwa mchango wao ni muhimu katika kuhakikisha tukio hilo linaipa Tanzania heshima na kuitangaza kimataifa.
Amewahimiza waandishi wa habari kuendelea kuandika na kusambaza taarifa zinazotangaza vivutio, fursa na mafanikio ya Tanzania, hususan katika sekta ya utalii.
Akizungumzia umuhimu wa sekta hiyo, amesema kuwa utalii una mchango mkubwa katika uchumi wa nchi, huku akieleza kuwa lengo ni kuongeza mchango wake katika pato la taifa.
“Kwa sasa sekta ya utalii inachangia asilimia 26 ya pato la Serikali. Malengo yaliyopo ni kuhakikisha sekta hii inachangia zaidi ya asilimia 45,” amesema.
Amesisitiza kuwa kufikiwa kwa malengo hayo kunahitaji ushirikiano wa wadau wote katika kuitangaza Tanzania, kuendeleza utamaduni wa ukarimu, kuimarisha upendo na kuhakikisha wageni wanaopokelewa nchini wanapata huduma na mapokezi mazuri.

Mkutano wa 153 wa IPU unatarajiwa kuileta Tanzania katika jukwaa la kimataifa, huku jijini Arusha likipata fursa ya kuonyesha uwezo wake wa kuandaa mikutano mikubwa ya kimataifa na kutangaza vivutio vyake vya utalii pamoja na fursa za uwekezaji na biashara.
Mwisho..
