ARUSHA YAWAKARIBISHA WAJUMBE 400 KUTOKA NCHI 48 KWA MKUTANO WA CATA WAJUMBE 400 KUTOKA NCHI 48 KUTUA.

Geofrey Steven
4 Min Read

Na Geofrey Stephen Arusha

Zaidi ya wajumbe 400 kutoka mataifa 48 wanatarajiwa kuwasili jijini Arusha kuhudhuria Mkutano wa 46 wa Wakuu wa Mamlaka za Mapato wa Jumuiya ya Madola (CATA), unaotarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, amesema hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mkutano huo, ambao sehemu kubwa ya shughuli zake itafanyika katika Hoteli ya Grand Melia Arusha.

 

Habari Picha 21546

CPA Makalla amesema maandalizi ya mkutano huo yamekamilika, huku akiahidi kuwa wageni watakaofika jijini Arusha watapata usalama na mazingira mazuri wakati wote wa ziara yao.
Ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuaminiwa kuwa mwandaaji na mwenyeji wa mkutano huo, akisema tukio hilo ni fursa muhimu kwa Tanzania kujifunza na kubadilishana uzoefu na mataifa mengine katika masuala ya ukusanyaji wa mapato.

TEKNOLOJIA KUWA AJENDA MUHIMU.

Kwa mujibu wa CPA Makalla, kaulimbiu ya mkutano huo inalenga matumizi ya teknolojia katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.

Amesema Tanzania itapata fursa ya kujifunza mifumo na mbinu mbalimbali zinazotumiwa na mamlaka za kodi za nchi nyingine, hususan katika matumizi ya teknolojia, uchambuzi wa taarifa na ubunifu wa huduma kwa walipakodi.
“Mkutano huu utaiwezesha TRA kubadilishana uzoefu kuhusu usimamizi wa kodi, ukusanyaji wa mapato, matumizi ya teknolojia katika uchambuzi wa taarifa pamoja na ubunifu katika utoaji wa huduma kwa walipakodi,” amesema CPA Makalla.

Ameongeza kuwa ushiriki wa wataalamu kutoka mataifa mbalimbali utasaidia kujenga uwezo wa wataalamu wa Tanzania na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya kodi, hasa wakati biashara zinazovuka mipaka zikizidi kukua.

ARUSHA KUNUFAIKA NA WAGENI.

CPA Makalla amewataka wananchi na watoa huduma jijini Arusha kutumia fursa hiyo kuwahudumia wageni kwa ukarimu na upendo.

Amesema wajumbe hao watatumia hoteli, usafiri na huduma mbalimbali wakati wa kukaa jijini Arusha, hivyo tukio hilo linaweza kutoa fursa kwa wafanyabiashara na watoa huduma kupata manufaa ya kiuchumi.

Habari Picha 21550

Ameeleza kuwa huduma bora kwa wageni inaweza kuwavutia kurejea Tanzania kwa shughuli nyingine, ikiwemo utalii na uwekezaji.
Aidha, amesema mkutano huo ni fursa ya kuitangaza Tanzania kimataifa na kuonyesha uwezo wa nchi kuandaa mikutano mikubwa ya kimataifa.

Kwa upande wa utalii, CPA Makalla amesema Arusha itapata nafasi ya kutangaza vivutio vya Tanzania, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na Mlima Kilimanjaro.

MAKAMU WA RAIS KUFUNGUA MKUTANO.

CPA Makalla amesema Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na kufungua mkutano huo Oktoba 6, 2026, jijini Arusha.

Habari Picha 21552

MASUALA YA KODI ZA KIMATAIFA KUJADILIWA.

Kwa upande wake, Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Mcha Hassan Mcha, amesema mkutano huo utajadili pia masuala ya kodi za kimataifa, ikiwemo namna ya kushughulikia kampuni zinazofanya biashara katika nchi zaidi ya moja.
Amesema wataalamu watabadilishana uzoefu kuhusu namna bora ya kutoza kodi kwa kampuni za kimataifa zinazofanya shughuli katika mataifa mbalimbali, huku wakizingatia mifumo na taratibu zinazokubalika kimataifa.

Mcha amesema huduma kwa walipakodi pia itakuwa miongoni mwa maeneo yatakayojadiliwa, kwa lengo la kujifunza uzoefu kutoka nchi nyingine na kuendelea kuboresha huduma zinazotolewa na TRA.

Habari Picha 21547

Aidha, amesema mkutano huo utajadili uchumi wa kidijitali na biashara zinazofanyika kupitia mitandao, pamoja na kubadilishana ujuzi na uzoefu kuhusu namna mamlaka za kodi zinavyoweza kukabiliana na changamoto zinazotokana na maendeleo ya teknolojia.

Habari Picha 21548

Kwa ujumla, mkutano huo unatarajiwa kuwa jukwaa la kubadilishana uzoefu, kujenga uwezo wa wataalamu wa kodi na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika ukusanyaji na usimamizi wa mapato.

 

Mwisho..

Share This Article
Leave a Comment