Na Geofrey Stephen Arusha .
Serikali imesema Mkutano wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (C-CEOs Forum) 2026 utakuwa jukwaa muhimu la kuimarisha utendaji, tija na mchango wa Mashirika ya Umma katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kampuni ya Matangazo inayo wezesha mkutano huo katika maswala muhimu ya Matangazo D& G LIMITED .
Mkutano huo utafanyika Septemba 28 hadi 30, 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), ukiwakutanisha viongozi kutoka Mashirika zaidi ya 300 ya Umma, wawakilishi wa sekta binafsi na wadau wengine zaidi ya 700.

C-CEOs Forum, unaoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), ni mkutano wa nne tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023. Unalenga kujadili namna ya kuongeza ufanisi wa Mashirika ya Umma na kuhakikisha mipango yao inaendana na vipaumbele vya Dira 2050.
Makalla: Arusha iko tayari kuwapokea washiriki.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, amesema mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa na Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi.
Makalla amesema mkutano huo utatoa fursa kwa viongozi wa Mashirika ya Umma kubadilishana uzoefu, kujenga ushirikiano na kutafuta njia za kuongeza tija.
Amesema pia ujio wa washiriki zaidi ya 700 utatoa fursa kwa sekta za hoteli, migahawa, usafiri, utalii, biashara na huduma nyingine.
«“Tunataka mkutano huu uwe na manufaa yanayoonekana pia nje ya ukumbi wa mikutano, kwa kuwafungulia fursa wafanyabiashara, watoa huduma na wananchi wa Arusha,” amesema Makalla.»
Amesisitiza umuhimu wa wakazi na watoa huduma wa Arusha kuwa wakarimu kwa wageni ili kujenga mazingira yatakayowavutia kurejea.
Mchechu: Mashirika ya Umma yalenge matokeo
Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema utekelezaji wa Dira 2050 unahitaji Mashirika ya Umma kubadili mtazamo kutoka kuendesha shughuli pekee na kuelekea katika kuzalisha matokeo yanayopimika na yenye thamani kwa Taifa.
Amesema ufanisi unatakiwa kuonekana katika matumizi bora ya rasilimali, ushindani, uimara wa kifedha na ubora wa huduma.

«“Tunataka Mashirika ya Umma yenye ufanisi wa juu, shindani na imara katika kutekeleza Dira 2050,” amesema Mchechu.»
Uwekezaji wa Serikali wafikia Sh92.28 trilioni
Mchechu amesema thamani ya uwekezaji wa Serikali katika Mashirika na kampuni zake imeongezeka kutoka Sh67.95 trilioni mwaka 2020/21 hadi Sh92.28 trilioni mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 35.8.
Amesema mafanikio hayapaswi kupimwa kwa gawio pekee, bali pia kwa kuangalia tija, ubora wa huduma, uimara wa kifedha, ubunifu, matumizi ya teknolojia, ajira, uzalishaji na mchango katika uchumi.
Mapato yasiyo ya kodi yaongezeka
Kwa mujibu wa Mchechu, mapato yasiyo ya kodi yanayotokana na Mashirika na taasisi zinazochangia kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina yameongezeka kutoka Sh637.7 bilioni mwaka 2020/21 hadi Sh1.327 trilioni mwaka 2025/26, sawa na ongezeko la asilimia 108.3.
Amesema mjadala kuhusu Mashirika ya Umma unapaswa kuangalia pia thamani pana inayozalishwa kupitia huduma, ajira, uzalishaji, ubunifu na mchango katika uchumi.
Teknolojia na AI kupewa nafasi
Mchechu amesema Mashirika ya Umma yanahitaji uongozi wa kimkakati, utawala bora na matumizi zaidi ya teknolojia za kidijitali na akili bandia (AI).
Pia amesisitiza uwekezaji katika rasilimali watu na ujuzi wa baadaye, mifumo endelevu ya fedha na ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, huku yakizingatia masuala ya mazingira, jamii na utawala bora (ESG).

Kwa ujumla, C-CEOs Forum 2026 inalenga kujadili namna ya kubadilisha rasilimali na uwekezaji wa Serikali kuwa utendaji, tija na matokeo yenye thamani zaidi kwa Taifa, huku Arusha ikitarajiwa kunufaika kiuchumi kutokana na ujio wa mamia ya washiriki.
Mwisho.
