Na Geofrey Stephen .
KARATU, ARUSHA
Wananchi wa Kata ya Baray, Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, wameanza kunufaika na upatikanaji wa maji ya umwagiliaji baada ya kuchimbwa kwa visima 11 katika kipindi cha takribani wiki mbili, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji wa kilimo na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.
Uzinduzi wa visima hivyo umefanyika katika kijiji cha Mangora, ambapo wananchi walionyesha furaha baada ya maji kupatikana, wakisema hatua hiyo itawasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao, hususan vitunguu ambavyo ni miongoni mwa mazao muhimu yanayolimwa katika eneo hilo.

Kata ya Baray ni miongoni mwa maeneo yenye shughuli kubwa za kilimo cha vitunguu, ambavyo huzalishwa kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi. Wananchi wameeleza kuwa upatikanaji wa maji ya uhakika utawasaidia kupunguza utegemezi wa mvua na kuongeza uzalishaji wa kilimo cha umwagiliaji.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Karatu Dkt Lameck Karanga amesema upatikanaji wa maji hayo ni sehemu ya utekelezaji wa juhudi za Serikali za kuhakikisha wakulima wanapata huduma muhimu kwa ajili ya kuongeza tija katika kilimo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, Wilaya ya Karatu inatarajiwa kuwa na jumla ya visima 30, vitakavyochimbwa katika kata tano, huku visima 11 tayari vikiwa vimechimbwa na kazi nyingine zikiendelea.
Mradi huo unatarajiwa kuwafikia takribani wakulima 830 na kuwezesha umwagiliaji wa zaidi ya ekari 1,200. Aidha, fursa za ajira zinatarajiwa kuongezeka, huku takribani ajira 180 zikitarajiwa kutokana na shughuli mbalimbali zitakazotokana na uwepo wa maji kwa ajili ya kilimo.
Mbali na visima, mradi huo unahusisha pia ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji, ikiwemo mabomba yenye kipenyo cha inchi nane na inchi sita, pamoja na miundombinu mingine itakayowawezesha wakulima kufikisha maji katika maeneo ya uzalishaji.

Diwani wa Kata ya Baray, Yasini Rashid Kasia, ameeleza kuwa wananchi wamepokea kwa furaha hatua hiyo, akisema upatikanaji wa maji utakuwa chachu ya kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha ya wakazi wa kata hiyo.
Amesema wananchi wa Baray wana matumaini makubwa kwamba kilimo cha umwagiliaji kitakapopanuka, uzalishaji wa vitunguu na mazao mengine utaongezeka na hivyo kutoa fursa zaidi za biashara na ajira kwa vijana.

Kwa upande wa utekelezaji, wataalamu wameeleza kuwa visima vilivyochimbwa hadi sasa vimeonyesha uwepo wa maji katika kina kinachotofautiana kulingana na eneo, kuanzia takribani mita 20 hadi zaidi ya mita 100.
Kata ya Baray ni miongoni mwa kata tano zitakazonufaika na mpango huo katika Wilaya ya Karatu. Kata nyingine ni Mangola, Daa, Rotia na Enamaga, ambapo vijiji mbalimbali vitanufaika na uchimbaji wa visima hivyo.
Viongozi wa Wilaya ya Karatu wameahidi kuendelea kusimamia na kulinda miundombinu hiyo, huku wananchi wakitakiwa kuitunza na kuhakikisha maji yanatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, hususan katika kuongeza uzalishaji wa kilimo.

Kwa wananchi wa Mangola na maeneo jirani, upatikanaji wa maji hayo umefungua ukurasa mpya katika kilimo cha umwagiliaji, huku matumaini yakielekezwa kwenye ongezeko la uzalishaji, kipato na ajira kwa vijana.
Mwisho.
