WANANCHI SIHA WAONYWA: KIFUNGO CHA MIEZI 6 KWA KUPIGA SIMU YA UONGO 114 – JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI LAPOKEA GARI JIPYA LA LITA 7,000

Geofrey Stephen
2 Min Read

Na Bahati Siha .

Wananchi wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro wameonywa kuwa watakaotoa taarifa za uongo kwa kupiga namba 114 ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wanaweza kukumbana na adhabu ya kifungo cha hadi miezi sita jela.

Onyo hilo limetolewa Februari 17 na Mkuu wa Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Siha, Paul Margwa, wakati wa kikao maalum cha Baraza la Madiwani kupitia mpango wa Bajeti ya Halmashauri kwa mwaka 2025/2026 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Margwa aliishukuru Serikali kwa kuipatia wilaya hiyo gari jipya la zimamoto lenye ujazo wa lita 7,000, akisema lilikuwa ni hitaji la muda mrefu kwa wananchi wa Siha.

Habari Picha 7235
Habari Picha 7234

Alifafanua kuwa hapo awali, pindi janga la moto lilipotokea, gari la zimamoto lililazimika kutoka Moshi Mjini na kuchukua muda mrefu kufika Siha, hali iliyokuwa ikiathiri ufanisi wa huduma. Kupatikana kwa gari hilo sasa kutarahisisha utoaji wa huduma kwa wakati.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa namba 114 itumike kwa dharura halisi tu na kuonya dhidi ya majaribio au taarifa za uongo, akisema kufanya hivyo kunaweza kusababisha hasara na kuchelewesha huduma kwa wahitaji halisi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Siha, Dancan Urasa,

aliwapongeza wataalamu wa Halmashauri kwa kuandaa bajeti inayozingatia mahitaji muhimu ya wananchi katika kila kata.
Aidha, alieleza kuwa Halmashauri imejipanga kuhakikisha ifikapo mwaka 2027 wanafunzi watakaomaliza darasa la sita wanapata miundombinu bora ya kuendelea na elimu ya sekondari, ikiwemo madawati, vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na walimu wa kutosha

Habari Picha 7236
Habari Picha 7237

Masuala ya umwagiliaji pia yalisisitizwa, huku ikitolewa rai kwa Tume ya Umwagiliaji kushirikiana na Halmashauri kukarabati mifereji ili kuboresha upatikanaji wa maji na kuimarisha kilimo cha umwagiliaji kama njia ya kukuza uchumi wa familia na Taifa kwa ujumla

Mwisho….

Share This Article
Leave a Comment