HAI YAZINDUA UANDIKISHAJI NA UGAWAJI WA VITAMBULISHO VYA NHIF: KAYA 3,220 KUNUFAIKA NA BIMA YA AFYA KWA WOTE.

Geofrey Stephen
2 Min Read

Na Bahati Hai.

Jumla ya kaya 3,220 katika Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro zimeanza kunufaika na Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote kupitia NHIF, ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya Bima ya Afya kwa wote.

 

Habari Picha 7242
Habari Picha 7241

Akizungumza Februari 19, 2026 wakati wa uzinduzi wa uandikishaji na ugawaji wa vitambulisho vya bima hiyo uliofanyika katika Shule ya Msingi Kibaoni, Bomang’ombe, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Hassani Bomboko, alisema kuwa wilaya hiyo ina takribani kaya 6,800 zilizo kwenye mpango wa TASAF, ambapo kaya 3,220 zimeanza kupatiwa bima ya afya inayolipiwa na Serikali.

Bomboko alisema gharama ya bima hiyo ni shilingi 150,000 kwa kaya kwa mwaka, na kwamba Serikali imechukua jukumu la kulipia gharama zote ili kuwawezesha wananchi wasiojiweza kupata huduma za matibabu kwa kipindi cha mwaka mzima.
Alimpongeza Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza dhamira yake ya kuanzisha mfuko wa bima ya afya kwa Watanzania wote, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kulinda nguvu kazi ya Taifa na kusaidia makundi maalumu wakiwemo wazee, watoto na watu wenye ulemavu, pamoja na kaya zisizojiweza zilizo kwenye mpango wa TASAF.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Hai, Itikija Msuya, alisema ugawaji wa vitambulisho kwa wanufaika wa TASAF utafanyika kwa siku mbili, kuanzia Februari 19, 2026, na kuendelea katika maeneo mengine ili kuhakikisha wote wenye sifa wanapatiwa vitambulisho.

Alieleza kuwa wanufaika watakapopata vitambulisho hivyo wataweza kupata huduma za afya katika ngazi zote za vituo vya afya, kuanzia zahanati, vituo vya afya hadi Hospitali ya Wilaya.

Habari Picha 7243
Habari Picha 7244

Naye Filipo Mssawa, mkazi wa Kambi ya Raha, Kata ya Muungano na mmoja wa wanufaika, alisema mpango huo umekuwa msaada mkubwa kwake, hasa ikizingatiwa kuwa amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya macho kwa muda mrefu na kushindwa kumudu gharama za matibabu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Hai, Dionis Myinga, alisema Halmashauri imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha kuhusu mpango huo na kusimamia kikamilifu utekelezaji wake ili walengwa wote wanufaike ipasavyo.
Mwisho.

Share This Article
Leave a Comment